Viongozi kupata zaidi mafunzo ya kuwajengea uwezo

0

Na. James K. Mwanamyoto, Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani amedhamiria kuendelea kutoa kipaumbele cha kuwapatia mafunzo viongozi ili kuwajengea uwezo kiutendaji, utakaowawezesha kumsaidia vema jukumu la kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo.

Mhagama ameeleza dhamira hiyo ya Rais, wakati akifunga mafunzo ya Sanaa ya Uongozi (The Art of Leadership) kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) yaliyotolewa na Taasisi ya UONGOZI jijini Dodoma.

Waziri alisema, mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuapa na kuanza kulitumikia Taifa, moja ya eneo ambalo alielekeza lipewe kipaumbele ni kutoa mafunzo kwa viongozi akitambua kuwa mafunzo ndio njia pekee ya kuwawezesha viongozi kuwa na ufanisi kiutendaji, hivyo ofisi yake imetekeleza kwa vitendo agizo hilo kwa kuwapatia mafunzo wajumbe wa kamati ya USEMI.

“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ana maono na ndio maana anatambua kuwa sisi tuliopewa dhamana ya kuwa viongozi tunahitaji kujengewa uwezo ili kupata ujuzi utakaoendana na mazingira yaliyopo ikiwa ni pamoja na kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia,” Mhagama alifafanua.

Kwa upande wake, mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya USEMI, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Makete, Festo Sanga alisema toka awe Mbunge hajawahi kupata mafunzo mazuri ya uongozi kama ambayo Taasisi ya UONGOZI imewapatia kwani yamemjengea uelewa kwenye eneo la akili hisia (emotional intelligence) utakaomuwezesha kuzungumza vizuri na wananchi na kupokea yale ambayo wananchi anaowaongoza wanahitaji kutekelezewa.

“Mafunzo haya kama Mbunge na Mjumbe wa kamati ya USEMI yamekuwa na manufaa makubwa kwani yamenipatia elimu ya namna ya kuisaidia Serikali katika ufuataliaji wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, pamoja na kusimamia matumizi ya fedha za umma ambazo Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikizitoa katika maeneo mbalimbali nchini ili kuleta maendeleo,” alisisitiza Sanga.

Naye, Dkt. Alice Kaijage ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya USEMI alisema, kwa ujumla wajumbe wote wa kamati ya USEMI waliopatiwa mafunzo wameridhika na maudhui ya mafunzo na kushauri yaendelee kutolewa kwa muda mrefu zaidi ili viongozi wapate ujuzi utakaowaongezea ufanisi kiutendaji.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) wamepatiwa Mafunzo ya Sanaa ya Uongozi (The Art of Leadership) na Taasisi ya UONGOZI kwa muda wa siku mbili, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuitaka taasisi hiyo kuendelea kuwajengea uwezo viongozi ili wawe na tija katika maendeleo ya taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here