Watoto 40 wafanyiwa upasuaji wa moyo JKCI

0

Na Mwandishi Maalum, Dar Es Salaam

WATOTO 40 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu wamefanyiwa upasuaji kwenye kambi maalum ya matibabu iliyomalizika jana katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.

Kambi hiyo ya siku tano ilifanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Mending Kids la nchini Marekani.

Kwa watoto hawa kufanyiwa upasuaji huu hapa nchini Serikali imeweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni moja fedha ambazo zingelipwa kama upasuaji huo ungefanyika nje ya nchi.

Akizunguma za waandishi wa habari jana jijini Dar Es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kati ya watoto 40 waliofanyiwa upasuaji 20 walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na 20 walifanyiwa upasuaji kwa njia ya tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab.

Dkt. Kisenge alisema, tangu waanze kushirikiana na shirika hilo la Mending Kids jumla ya kambi sita za matibabu ya moyo kwa watoto zimeshafanywa huku wataalamu wa JKCI wakifundishwa njia mbalimbali za kufanya upasuaji wa kufungua kifua na ule wa tundu dogo kwa utaalam zaidi.

“Kupitia Shirika la Mending Kids wataalam wa JKCI wa upasuaji wa moyo kwa watoto wamekuwa mabingwa wabobezi katika kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto wenye magonjwa ya moyo hivyo kutufanya kuwa mabingwa kusini mwa jangwa la Sahara katika kutoa huduma bora za matibabu ya moyo kwa watoto,” alisema Dkt. Kisenge.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mending Kids Isabelle Fox alisema anafurahi kuona utaalamu wa wataalam wa JKCI umekuwa ukiongozeka kila siku ambapo kwa sasa wanaweza kufanya upasuaji wa aina mbalimbali wa moyo tofauti na walivyoanza kushirikiana mwaka 2015.

“Katika kambi hii pamoja na kufanya upasuaji wa moyo tumekuwa tukitoa mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo wataalamu wa Taasisi hii ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kuokoa maisha ya watoto wenye matatizo ya moyo ili waweze kuendelea na maisha kama watoto wengine na kuwarejeshea tabasamu”, alisema Isabelle.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here