Na Mwandishi Wetu
BALOZI wa Uholanzi nchini Wiebe Jakob de Boer amesema, waandishi wa habari ndio walinzi wa demokrasia kwenye Taifa lolote duniani.
Alisema hayo wakati akifungua semina ya kuwajengea uwezo waandishi kuhusu mabadiliko ya sheria ya habari nchini, iliyoandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), na kufanyika katika Hoteli ya Slip Way, jijini Dar es Salaam.
Balozi Boer alisema, ni ukweli ulio wazi kwamba, vyombo vya habari huru ndio msingi wa kuibua mijadala mizito na hutoa mwongozo katika utungaji wa sheria na mwelekeo chanya wa Taifa.
Alisema, uhuru wa vyombo vya habari ndio moyo wa demokrasia ya nchi yoyote kwa kuwa, hutoa mwanga na mwelekeo wa Taifa.
Mbali na hilo, balozi huyo aliipongeza TEF kwa kuandaa programu za kuwajengea uwezo wanahabari ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi zaidi, huku akiweka wazi kwamba, ubalozi wa Uholanzi upo tayari kusaidia TEF katika mipango yake.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile alimweleza Balozi Boer kuhusu utayari wa Serikali katika safari ya mabadiliko ya sheria ya habari.
Alieleza mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari unahusisha taasisi mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jamii Forums.