OWMS yamaliza migogoro na wawekezaji, wafanyabiashara kwa njia ya majadiliano

0

Na Mwandishi Wetu, OWMS, Dodoma


OFISI ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) imeendelea kuiwasilisha Serikali katika kusimamia mashauri ya madai na usuluhishi ambapo imefanikiwa kuendesha mashauri ya madai na usuluhishi 6,043 kwa kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwa OWMS mwaka 2018.


Hayo yameelezwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende wakati akizindua Baraza la kwanza la wafanyakazi wa OWMS lililofanyika jijini Dodoma na kusema kuwa OWMS imeendesha mashauri hayo kwa niaba ya Serikali kwa umakini mkubwa na umahiri ili kuendelea kutekeleza majukumu ya OWMS ili kufikia na hata kuzidi matarajio ya Serikali.


Aliongeza kuwa, OWMS imeendelea kuiwakilisha Serikali Mahakamani na katika mabaraza ya usuluhishi ambapo tangu kuanzishwa kwake imeendesha mashauri ya madai yapatayo 5,885 na mashauri ya usuluhishi 158 na kufanya jumla ya mashauri kuwa 6,043.


“Mashauri ya Madai yaliyomalizika katika kipindi cha miaka minne ni mashauri 582 na ya Usuluhishi ni mashauri 60 ambapo kati ya hayo, Serikali imeshinda mashauri 530 ya madai na Mashauri ya Usuluhishi 31”, alisema Dkt. Luhende.


Alisema, kama alivyoagiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, OWMS imeendelea kuhakikisha inaiwakilisha vyema Serikali na kuvutia wawekezaji nchini kwa kumaliza migogoro mbalimbali dhidi ya wawekezaji na wafanyabiashara kwa njia ya majadiliano.


Dkt. Luhende alisema, utaratibu huo umesaidia kupunguza idadi ya migogoro dhidi ya Serikali iliyofunguliwa kwenye Mahakama na mabaraza nje na ndani ya nchi; kuokoa fedha za Serikali ambazo zingetumika katika kuendesha migogoro tajwa; kudumisha uhusiano kati ya Serikali na wawekezaji; kujenga imani kwa wawekezaji kuhusu hali ya utoaji haki nchini; na kukuza diplomasia ya uchumi.


“Mfano wa shauri la usuluhishi lililomalizika kwa njia ya majadiliano ni baina ya G.S Engineering &Construction Corporation ya Korea ya Kusini dhidi ya TANROADS likihusiana na ujenzi wa daraja la Tanzanite na mgogoro ulikuwa umepelekwa ICC na shauri lilimalizika na sasa daraja linaendelea kutoa huduma kwa wananchi,” alisema Dkt. Luhende.


Pia, amewapongeza watumishi wa OWMS ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa ufanisi ili kuhakikisha maslahi ya Taifa yanalindwa kwa ulinzi mkuu pamoja na kukuza diplomasia ya uchumi wa nchi.


Mmoja wa Wajumbe wa Baraza hilo, Wakili wa Serikali, Rashid Mohamed alisema, siri ya mafanikio yaliyopatikana ni uongozi thabiti wenye kutoa maelekezo sahihi ya namna ya kutekeleza majukumu ya Ofisi ambapo Mawakili wenyewe wamekuwa na jitihada za kujifunza kile wanachokifanyia kazi ili kuweza kuleta mafanikio kwenye kazi wanazozifanya.


Naye Wakili wa Serikali Mwandamizi, Jenipher Kaaya ambaye pia ni mjumbe wa Baraza hilo alisema, OWMS inafanikiwa kumaliza mashauri nje ya mahakama au mabaraza ya usuluhishi kwa kufanya majadiliano na wale wanaoidai Serikali kwa kuweka masuala ya kisheria pembeni na kujadili hoja kama watu wa kawaida na hatimaye kufika mwafaka na kuweza kushinda mashauri hayo.


“Katika majadiliano hayo kuna sehemu kadhaa tunatumia sheria kwa kutegemeana na aina ya kesi na hivyo kwa kutumia usuluhishi tumefanikiwa kumaliza migogoro mingi kwa wakati na kwa muda mfupi tofauti na mahakamani ambapo historia inaonyesha kuwa migogoro inakaa mwaka mmoja au miaka miwili tu na kumalizika,” alifafanua Kaaya.


Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa OWMS, James Kibamba ametoa rai kwa wajumbe hao kuhakikisha kuwa masuala wanawakilisha vema watumishi wengine na kuwapatia mrejesho kwa kuwa sio rahisi kwa watumishi wote kuwa wajumbe wa Baraza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here