SHAKA: CCM itashirikiana na kila mwenye nia njema ya kuleta maendeleo

0

Na Peter Lyowa

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Shaka Hamdu amesema, chama hicho kipo tayari kushirikiana na yeyote au kikundi chochote chenye nia njema ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuharakisha maendeleo ya nchi na watanzania kwa ujumla.


Shaka alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Viongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Mkoa wa Dodoma (DWJ) waliomtembelea ofisini kwake, Makao Makuu ya CCM Jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha, kueleza kazi wanazozifanya na kuomba ushirikiano.


Aidha, aliwapongeza DWJ kwa kuijunga katika umoja na kufanya kazi za kurejesha kwa jamii huku akiwapa shime ya kutumia kalamu na taaluma zao kueleza mafanikio ya utendaji wa Serikali ya CCM Awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.


“Nawapongeza kwa kujiunga katika umoja wenu pamoja na kazi mnazozifanya za kugusa maisha ya jamii hususani watu walio katika mazingira magumu kama vile mayatima, wagonjwa, wahitaji wengine pamoja na uhifadhi wa mazingira. Nawahakikishia CCM tutawaunga mkono,” alisema.


Aliendelea kusema “Ombi langu kwenu pamoja na kazi nzuri ya uandishi wa habari mnayoifanya nawaomba andikeni kuhusu kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ili jamii ijue nini Serikali yao inafanya na kuwanyima fursa wapotoshaji kupata himaya kwenye jamii yetu.”


Shaka alisisitiza kwamba, ni vyema jamii yetu ikaunga mkono watu au vikundi vinavyojitoa kuunga mkono juhudi za serikali za kuharakisha maendeleo na kutoa huduma kwa jamii ili kuwatia moyo lakini pia ikiwa ni sadaka.


Kwa sasa DWJ inawahudumia wanafunzi watano wa kidato cha 5 na sita, inahudumia mwanamke mmoja mtu mzima mwenye tatizo la mifupa aliyelazwa taasisi ya mifupa Muhimbili (MOI) na wanatekeleza programu ya upandaji miti jiji la Dodoma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here