Kuna nini nyuma ya mgomo
wa mchezaji Mussa Kamara?

0

Na Mwandishi Wetu

WAKATI wachezaji wengi barani Afrika wamekuwa na ndoto ya kwenda kucheza soka la kulipwa Barani Ulaya, hali ni tofauti kwa mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Sierra Leone, Musa Noah Kamara, maarufu kama ‘Musa Tombo’ ambaye amegoma kwenda kucheza soka nje ya nchi yake.

Kamara ambaye yupo chini ya wakala Roland Ekokobe, amesema hataki kutoka nje ya nchi hiyo, sio kwasababu hana uwezo wa kwenda kucheza soka la kulipwa popote pale dunianu, bali ana sababu zake binafsi.

Itakumbukwa, mchezaji huyo mwenye kipaji kikubwa cha kucheza soka, aliwahi kusaini mkataba na klabu ya Trelleborgs FF ya nchini Sweden, lakini alivunja mkataba muda siku chache baadae na kurudi nchini kwao.

Inaelezwa, mchezaji huyo alidai kwamba, kutokana na changamoto za kiafya zinazomkabili, hatoweza kucheza soka nchini humo kwani kuna baridi kali, hivyo wakala wake aliamua kumrudisha Sierra Leone.

Mbali na mkataba huo, Kamara ameshindwa kucheza soka Norway baada ya wakala mmoja kujitokeza na kumpeleka nchini humo na alijiunga na moja ya klabu zinazoshiriki Ligi Kuu.

Taarifa zinadai kwamba, mchezaji huyo alisajiliwa bila kufanyiwa majaribio kutokana na uwezo mkubwa wa kucheza soka, na baada ya siku moja akaanza kulia na kulalamika akitaka arudishwe kwao.

Hata hivyo, licha ya wakala aliyempeleka kudai aachwe ili azoee hali hiyo, lakini mwenyewe alitishia kujinyonga iwapo hatarudishwa kwao, jambo ambalo liliwalazimu waliohusika na uhamisho wake kumrudisha Sierra Leone.

Aidha, baadae wakala wake aliona huenda labda mchezaji huyo anaweza kucheza kwenye klabu zilizopo Afrika, hivyo aliamua kufanya mazungumzo na klabu ya Al – Ittihad Tripoli ya Libya, na tayari amejiunga nao, lakini tayari ameomba arudishwe nchini mwao.

Moja ya madai aliyotoa safari hii ni kwamba, nyakati za usiku anasikia milio ya risasi nchini Libya, hivyo haoni kama kuna usalama wa kutosha huku akidai kwamba, iwapo atapoteza maisha akiwa nchini humo, mke wake na wakala wake Roland Ekokobe wanapaswa kubeba lawama, kwani hawataki arejee Sierra Leone.

Hadi sasa, wachambuzi wa masuala ya soka nchini mwao na duniani kote, wameshindwa kujua hasa kilichopo nyuma ya mgomo huo wa Mussa Kamara wa kukataa kwenda kusakata kabumbu nje ya nchi yake.

Wapo wanaodai huenda anasumbuliwa na matatizo ya akili au ana hofu ambayo inapaswa kuchunguzwa na kutafutiwa suluhu badala ya kuendelea kumtafutia timu nyingine, kwani kuendelea kufanya hivyo kunaweza kusababisha madhara makubwa zaidi; anaweza kujidhuru, ikizingatiwa mara kadhaa ametishia kufanya hivyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here