Kwanini wanawake wanatumiwa zaidi kwenye matukio ya ugaidi?

0

Nairobi, KENYA

KWENYE shambulizi la kigaidi lililofanyika Westgate Shopping Mall nchini Kenya miaka kadhaa iliyopita, vyombo vya usalama vilimtaja Samantha Lewthwaite mwenye kufahamika kwa jina la Mjane mweupe (White Widow) kuwa ndio alipanga njama zote za tukio hilo.

Samantha Lewthwaite alitajwa kushirikiana na Kundi la wapiganaji wa Al- Shabaab na alidaiwa kupotea muda mfupi baada jinai hiyo. Rekodi za usalama zinaonyesha, mwanamke huyo aliwahi kusafiri kutoka Afrika Kusini hadi Kenya kupitia Tanzania kisha akaelekea Somalia.

Vyombo vya habari vikanukuu Mashirika ya Kijasusi ya Magharibi yakidai, mwanamke huyo gaidi mwenye asili ya Ireland, Samantha Lewthwaite, atatiwa nguvuni wakati wowote ingawa hadi leo imepita miaka kadhaa, hawajafanikiwa kutimiza ahadi yao hiyo.

Baadae katika kuthibitisha kwamba mashirika hayo yameshindwa kumnasa, tukasikia habari kwamba mwanamke huyo gaidi anayeogopwa duniani kote, amefunga ndoa na mbabe mmoja wa vita nchini Somalia.

Gazeti la ‘Daily Mirror’ la nchini Uingereza likasema kwamba, mume wa sasa wa Mjane Mweupe ni mmoja wa makamanda wa juu kabisa wa kundi la Al- Shabaab, Hassan Maalim Ibrahim anayefahamika zaidi kama Sheikh Hassan.

Mama huyo mwenye watoto wanne, anadaiwa kwamba hivi sasa ni mmoja wa viongozi wakuu wa mipango wa kigaidi ya kundi la Al- Shabaab. Hiyo imekuwa ni ndoa ya tatu ya Mjane Mweupe na kwa ndoa hiyo, na hivi sasa anapewa ulinzi wa moja kwa moja kwa saa 24 na kundi la mumewe akiwa chini ya wapiganaji wenye silaha nzito.

Tangu kutokea kwa shambulizi kwenye maduka ya West Gate mjini Nairobi na mwanamke huyo kutajwa kama kinara wa mashambulizi hayo, Samantha amekuwa akisakwa na vyombo vyote vya ujasusi vya nchi wa magharibi na hivyo kumfanya aishi kwa maisha ya kuhamahama na kujificha.

Mwanzoni alikuwa akilindwa na kundi la wapiganaji wanaofahamika kama kikosi cha kujitoa muhanga, kilicho chini ya kundi Al-Qaeda. Alikuwa mke wa Germain Lindsay, mtu aliyelipua bomu kwa kujitoa mhanga nchini Uingereza na kuua watu 27 kwenye njia ya gari moshi la chini ya ardhi mwaka 2005.

Lewthwaite na Hassan walionekana kwenye kijiji cha Nasable kilichoko porini, kilomita 25 kutoka mji wa Baidoa mara baada ya kufunga ndoa. Gazeti la ‘Daily Mirror’ limesema taarifa lilizozipata kutoka ndani ya kundi hilo zimesema: “wakwe zake wanampa heshima kubwa kwa kuwa hivi sasa ni mmoja wa wanafamilia wao.

“Samantha yuko kwenye kijiji kinacholindwa vikali na yupo kwenye eneo ambalo wanaoruhusiwa kuingia ni watu maalum tu. Mpaka wakati huu, huwa hatoki kabisa kwenye nyumba ya nyasi anayoishi na mumewe. Anapotoka huvaa soksi na glavu nyeusi ili kuficha ngozi yake nyeupe. Kwa ndoa hii, Samantha amejipatia ulinzi mkubwa.”

Inaaminika kwamba Lewthwaite, ni miongoni mwa watu wanaopanga kulipa kisasi kutokana na kuuawa kwa Abubakar Shariff Ahmed. Ahmed aliuawa kwa bunduki wakati akiwa anatembea barabarani, mjini Mombasa nchini Kenya. Mara baada ya mauaji hayo, Vyombo vya usalama vya nchi za Magharibi vilieleza hofu yake kwamba huenda akaanza kuua watu wa magharibi na kuharibu rasilimali zao na kuilaumu serikali ya Kenya kwa kifo cha Ahmed.

Ahmed, ambaye alikuwa akikanusha kwamba aliwahi kukutana na Lewthwaite, alidaiwa kuwasaidia Waingereza zaidi ya 100 kujiunga na kundi la Al- Shabaab.

Ukiachana na habari za Mjane Mweupe, Januari 15 mwaka huu limetokea shambulizi jingine katika hoteli ya Dusit D2, ambapo vyombo vya usalama vimemtaja Violet Kemunto (Omwonyo) kuwa mwandaaji wa shambulizi na anadaiwa kushirikiana na Al- Shabaab. Violet ni mke wa Gaidi mwingine Ali Salim Gichunge.

Baba yake Ali ni mwanajeshi, pia alihojiwa kama ilivyo kwa ndugu zake. Gichunge alikuwa mfanyakazi wa mkahawa wa intaneti ndipo alikoanza mawasiliano na magaidi. Gichunge ni mzaliwa wa Isiolo eneo linalotumika kuchukua vijana wengi kwenda Somalia kujiunga na Al- Shabaab. Siku chache baada ya kuacha kazi polisi walizingira mkahawa huo na kuchukua kompyuta zote kwa tuhuma za kuhusika na ugaidi. Gichunge anadaiwa kuwaaambia wazazi wake (kwa simu) kuwa ataenda masomoni katika nchi za Uganda na Tanzania.

Haikuwa hivyo, badala yake alikuwa Mombasa ambako rafiki yake alimtafutia kazi. Siku chache baadaye akatoweka kwa rafiki yake. Ilimlazimu rafiki yake apige simu kwa wazazi wa Gichunge kuwaeleza hali halisi na hakuwa na mawasiliano nae.

Baadaye Gichunge alimpigia simu dada yake Amina Sheriff kumweleza yuko Lamu njiani kwenda nje ya Kenya. Simu aliyoitumia ilificha utambulisho wa namba. Dada yake ameviambia vyombo vya usalama kuwa anaamini safari yake Lamu ilikuwa kuelekea Somalia kwa Al- Ahabaab.

Tangu mwaka 2015 Gichunge alipotea na hakujulikana yuko wapi, hadi alipobambwa kwenye shambulizi la Nairobi. Anahisiwa kupata mafunzo huko Somalia. Violet anatajwa kusoma mawasiliano ya umma katika chuo cha MMUST. Naye kwa kipindi cha mwaka 2016 hadi 2017 alipotea, hakujulikana alipo. Hakuwawasiliana na mtu yeyote hadi pale alipojitokeza mwaka jana kuwa anafunga ndoa na Ali Gichunge.

Vyombo vya usalama vimeeleza kuwa, huenda aliondoka saa chache kabla ya shambulizi kuelekea Somalia. Polisi walisema wanamsaka mwanamke huyo kona zote za Kenya. Violet Kemunto ndiye anatajwa kumshawishi Gichunge kushiriki jinai za Al- Shabaab. Violet jina lake la utani ni ‘Al- Shabaab bride’.

Tangu lilipotokea tukio hilo, kumezuka mijadala mbalimbali wakihoji sababu za wanawake kuonekana kuwa mstari wa mbele katika kusuka mipango ya matukio ya kigaidi, wakirejea tukio la Mjane Mweupe na sasa Violet Kemunto. Wengi wanasema, wanawake wanatumika kwa sababu sio rahisi kutiliwa mashaka ndio maana wanafanikiwa kupanga na kufanikisha matukio yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here