NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha usanifu wa awali wa ujenzi wa barabara za njia nne zitakazoanzia Nanenane-Msamvu-Kihonda na kuanzia Msamvu hadi Semi mkoani Morogoro, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa magari katika mkoa huo.
Mhandisi Kasekenya ameyasema hayo Novemba 26, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Morogoro katika mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uliofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mkoani humo.
Ameongeza kuwa Serikali ina mpango wa kujenga barabara ya mchepuko (Bypass) itakayokuwa sehemu ya mradi wa barabara ya ‘Expressway’ kutoka Chalinze kuelekea Morogoro, ambapo barabara hiyo itaanzia Kingolwira kupitia Makunganya hadi Sangasanga na inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha njia nne au sita.
Amefafanua kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kupunguza changamoto ya foleni ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi pamoja na wadau wa usafirishaji katika Mkoa wa Morogoro.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Josephine Kapoma, amesema mkoa huo unahitaji kuendelea kuimarishiwa miundombinu ya barabara ili kuendana na mahitaji ya maendeleo na hadhi yake unapotarajiwa kuwa jiji.
Ameeleza kuwa mkoa huo umeshuhudia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuomba Serikali kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya barabara ili kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji.