Na Aisha Swahibu, WAF
MGANGA Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, amesema mafanikio ya sekta ya afya hayapaswi kupimwa kwa idadi ya vituo vilivyojengwa na watumishi walioajiriwa pekee, bali pia kwa ubora wa huduma zinazotolewa na namna zinavyokidhi mahitaji ya wananchi.
Akizungumza Novemba 6, 2026, jijini Dar es Salaam, katika kikao cha kupitia rasimu ya ajenda ya Mkutano wa Kitaifa wa Makubaliano kuhusu Afya (National Health Compact), amesema uwekezaji unaofanywa na Serikali unapaswa kuleta matokeo yanayoonekana katika kuboresha huduma na kuongeza kuridhika kwa wananchi.
“Tunamkumbuka Mheshimiwa Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, wakati anaingia Wizarani, msisitizo wake ulikuwa katika ubora wa huduma. Hivyo, kupitia makubaliano haya tunaweza kufikia maono ya Waziri wetu,” amesema Prof. Sunguya.
Amesema ni muhimu kuweka malengo mahsusi na yanayopimika yanayoendana na rasilimali zinazotarajiwa kupatikana ili kuhakikisha uwekezaji huo unaleta tija na kuboresha upatikanaji wa huduma bora na nafuu kwa wananchi.
Aidha, amesisitiza kuwa ufuatiliaji na tathmini vinapaswa kuanza tangu hatua za awali za utekelezaji kwa kuweka malengo, viashiria na muda maalumu wa kupima mafanikio badala ya kusubiri hadi mwisho wa utekelezaji.
Prof. Sunguya amehimiza matumizi ya tafiti, ushahidi na bunifu zinazozalishwa nchini katika kuboresha huduma za afya, akieleza umuhimu wa kufupisha muda wa matokeo ya tafiti kufikishwa katika sera na utekelezaji ili wananchi wanufaike kwa wakati.
Katika eneo la rasilimali watu, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mafunzo na kuhakikisha watumishi wa afya wanasambazwa kwa usawa kulingana na mahitaji ya maeneo mbalimbali nchini.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa umiliki wa ndani na ushirikishwaji wa wadau wote katika utekelezaji wa makubaliano hayo, akieleza kuwa mafanikio yake yanahitaji ushirikiano na uwajibikaji wa pamoja.
Ameongeza kuwa makubaliano hayo yanapaswa kuimarisha utoaji wa huduma jumuishi kuanzia ngazi ya huduma za afya ya msingi hadi hospitali za kibingwa na rufaa, sambamba na kuongeza kasi ya utekelezaji wa ajenda ya Serikali ya Afya kwa Wote (Universal Health Coverage – UHC).