Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema uamuzi Umoja wa Ulaya (EU) kurudisha rasmi upatikanaji fedha za Maendeleo kiasi cha Euro Milioni 156 (takriban Shilingi Bilioni 461 za Tanzania) ni fahari ya aina yake kimaendeleo.
Aidha, hatua hiyo imetajwa na CCM ni kutokana na kukubalika kwa diplomasia ya Tanzania chini ya Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, chama hicho kimesisitiza kuwa sifa za Tanzania mbele ya Mataifa yote ulimwenguni inafahamika kwa misimamo na sera zake katika kusimamia haki za binadamu
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa kamati maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya itikadi ,Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis Afisini kwake Kisiwandui kisiwani hapa.
Mbeto alisema, kuna baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani ambao hawaitambui historia yaTanzania Kimataifa, wamekuwa wakidhani wangeweza kuipaka matope Tanzania Kimataifa.
Alisema, licha ya kuwepo kwa baadhi ya mtu Wanasiasa na Wanaharakati makuwadi katika mawanda ya diplomasia na Siasa za Kimataifa ,ni wakati wao wa kujifunza na kuitambua heshima ya Tanzania mbele ya Jumuiya za kimataifa.
Aidha, chama hicho kimesisitiza kuwa sifa za Tanzania mbele ya ulimwengu zinafahamika ikiwa ni pamoja na misimamo,malengo na sere zake katika kusimamia haki za binadamu
“Tanzania inatazamika kutokana na heshima mbele ya macho ya ulimwengu miaka na miaka.Inasifika kwa kusimamia kwake Amani na umoja kitaifa, Ina sera makini, mipango na utashi katika kusimamia haki za binadamu,domokrasia na maendeleo,” alisema Mbeto.
Akifafanua zaidi, alisema juhudi uchwara za baadhi ya vyama vya upinzani vilivyokuwa vikitaka kuthubutu kuichafua nchi yetu, wao na mawakala wao wamejikuta wakigonga mwamba.
Mbeto alisema, kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Ushirikiano wa Umoja wa Ulaya EU nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Marc Stalmans, EU itaendelea na utoaji wa kiasi chote cha fedha.
“Tutaendelea kuaminika na kujiaminisha mbele ya ulimwengu.Tunasikilizwa kutokana na historia yetu na utendaji wetu mwanana. EU itaendelea kutoa fedha zote za maaendeleo bila kupunguza bajeti au kubadili malengo ya shughuli husika,” aliongeza.
Akielezea kwa undani, Katibu huyo Mwenezi alisema Umoja wa Ulaya mbali na kuwa Mdau na Mshirika mkubwa wa Maendeleo kwa Tanzania, ni kinara wa Ushirikiano wa Maendeleo ya kisekta.
“EU tumekuwa tukishirikiana na EU katika Sekta za Kilimo, Nishati, Miundombinu, Biashara na Teknolojia. Takwimu za EU zinaonesha kukua kwa Biashara baina ya pande mbili kwa Euro Bilioni 2.15 kwa mwaka,” alisisitiza Mbeto.