NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Damas Kamani, amezinadi fursa za uwekezaji katika sekta za mifugo na uvuvi wilayani Mufindi mkoani Iringa, akiwahimiza wawekezaji kutumia fursa zilizopo kuanzisha miradi ya kibiashara itakayoongeza uzalishaji, ajira na kukuza uchumi wa wananchi.
Kamani amezinadi fursa hizo wakati akifunga rasmi Maonesho ya Kwanza ya Biashara na Uwekezaji ya Wilaya ya Mufindi 2026, yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Wambi.
Amesema Wilaya ya Mufindi ina mazingira yanayofaa kwa ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa maziwa na nyama, mbuzi na kondoo, pamoja na ufugaji wa samaki kwenye mabwawa na vizimba, viwanda vya kuchakata maziwa na nyama, pamoja na uzalishaji wa chakula cha mifugo, kuku na samaki.
Ameongeza kuwa uwekezaji katika sekta hizo unapaswa kuleta manufaa kwa jamii kwa kuongeza ajira, kuimarisha usalama wa chakula na lishe, na kupanua masoko kwa wafugaji na wavuvi huku akiwahimiza wafugaji na wavuvi kutumia maarifa na teknolojia walizojifunza katika maonesho hayo kuboresha shughuli zao na kuhamia kwenye uzalishaji wa kibiashara.
Aidha, Naibu Waziri Kamani ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Mufindi ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt. Linda Salekwa, kwa kuja na maonesho hayo ambapo ameitaja kuwa ni hatua muhimu katika kutafsiri kwa vitendo Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 kupitia ubunifu, uzalishaji na uanzishaji wa fursa za ajira.