MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amepokea taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Nsalaga hadi Ifisi, yenye urefu wa Kilomita 29, kwa kiwango cha lami mkoani Mbeya.
Taarifa hiyo imetolewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta.
Mradi huo unaotekelezwa na Mkandarasi CHICO, chini ya usimamizi wa Mhandisi Mshauri TECU, umefikia asilimia 46 ya utekelezaji wake.
Mradi huo ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Jiji la Mbeya na maeneo jirani, kupitia uboreshaji wa miundombinu ya barabara ili kuongeza ufanisi katika usafiri na usafirishaji.
Aidha, kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha muunganiko wa usafiri kati ya mikoa ya Njombe, Mbeya na Songwe, pamoja na kuimarisha mawasiliano ya kibiashara na usafirishaji kati ya Tanzania na nchi jirani za Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Vilevile, barabara hiyo ni kiungo muhimu katika mtandao wa usafiri na biashara wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).