Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Waziri wa Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Omar Said Shaaban, kuacha drama za kisiasa, kikisema hana uwezo wa kukwepa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama kilichotoa Rais.
Pia, chama hicho kimemshauri Waziri huyo kusoma na kuielewa Ibara ya 9, Kifungu cha 2(a), cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kinachoeleza kuwa mamlaka ya kuongoza nchi yanatokana na wananchi wenyewe.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, ibara hiyo inaipa uhalali sera za CCM kutekelezwa na mawaziri, kwa sababu hakuna serikali inayokwenda kwenye uchaguzi, bali wananchi hutumia mfumo wa kidemokrasia kukichagua chama, kisha chama hicho ndicho kinachounda serikali.
Aidha, Rais aliyechaguliwa kupitia chama hicho ndiye msimamizi mkuu wa sera na ilani ya chama chake. Hivyo, waziri hawezi kukwepa kutekeleza maelekezo ya Rais, ambayo yanatokana na sera na ilani ya chama chake.
Akiendelea kutoa ufafanuzi huo, Mbeto alisema kuwa Ibara ya 39(5) ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, pamoja na mabadiliko yake ya kumi, inaeleza majukumu ya Makamu wa Kwanza wa Rais, akiwemo kutekeleza majukumu atakayopangiwa na Rais.
Alisema, Rais huyo ametokana na chama kilichoshinda uchaguzi na ndiye anayesimamia sera na ilani ya CCM. Kwa msingi huo, hata Makamu wa Kwanza wa Rais, ambaye ni bosi wa Waziri Omar, anapaswa kutekeleza majukumu na maelekezo anayopangiwa na Rais.
Ufafanuzi huo umetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, aliyemtaka Waziri Omar kuacha kutumia mbinu za kale na kufanya siasa nyepesi.
Alisema kitendo cha Waziri Omar kuonesha kutopokea Ilani ya CCM, ambayo ndiyo yenye miongozo ya utekelezaji wa misingi ya kisera, hakimpi nafasi ya kukwepa utekelezaji wa ilani hiyo.
“Si Waziri Omar peke yake, hata chama chake ACT hakithubutu kukwepa utekelezaji wa sera zilizoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Mpelekeeni salamu, kisha mwambieni aache siasa za danganya toto,” alisema Mbeto.
Aidha, katibu huyo wa uenezi alieleza kwa undani kuwa, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, chama kilichotoa Rais ndicho kitakachounda serikali na kusimamia utekelezaji wa sera zake.
“Makamu wa Kwanza wa Rais, Omar, na mawaziri wenzake kutoka ACT wameapishwa na Rais wa SMZ, Dk. Hussein Ali Mwinyi. Midhali wameapa mbele ya Rais kutoka CCM, watakwepaje, kwa mfano, utekelezaji wa ilani?” alihoji Mbeto.
Kwa upande mwingine, mwenezi huyo alisema huu ni wakati wa kufanya kazi za serikali na kuwatumikia wananchi. Hivyo, alimsihi Waziri Omar kuacha dhihaka na mzaha wakati wa kutekeleza majukumu ya umma.
“Macho ya wananchi wote yanaitazama Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyo chini ya Umoja wa Kitaifa. Wananchi wanataka kuwaona mawaziri wote wakichapa kazi bila kuamsha ngonjera za kisiasa,” alisisitiza.
Hata hivyo, Mbeto alisema Waziri Omar bado ana nafasi ya kuchukua hatua endapo haridhiki kufanya kazi chini ya Rais aliyeshinda uchaguzi na kumteua kushika nafasi hiyo. Alisema waziri huyo anaweza kumwandikia Rais barua ya kujiuzulu.
“Waswahili husema unaweza kumpeleka ngamia hadi kisimani, lakini huna uwezo wa kumlazimisha kunywa maji. Kuteuliwa ni haki ya msingi, na mteule kujiuzulu ni wajibu usio na taklifu,” alisema mwenezi huyo.
Kadhalika, Mbeto alisema tangu kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar mwaka 2010, mawaziri wote walioteuliwa hawajawahi kugomea kupokea Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ambayo imekuwa ikitumika katika utekelezaji wa shughuli za kiutendaji.