Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuundwa kwa Kamati ya Pamoja ya utekelezaji wa ajenda za tamko la pamoja la maridhiano ni suala la kisiasa, lakini ushiriki wa vyama vya Siasa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) ni sharti la Kisheria na Kikatiba.
Kwa muktadha huo, CCM imekitaka ACT Wazalendo kuanza kutekeleza wajibu wa kushiriki Serikalini wakati mpango wa kuundwa kwa Kamati ya pamoja ukiendelea kufanyika.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyesema Vyama vilivyokidhi matakwa ya sheria na kutakiwa kushiriki katika SUK ni faradhi.
Mbeto alisema, CCM na ACT vina wajibu na shuruti ya kushiriki kwenye Serikalini kutokana na mahitaji ya Katiba huku mchakato wa kuundwa kwa Kamati ya Pamoja ya Maridhaino, mchakato wake ukiendelea.
Aliwataka Viongozi wa ACT Wazalendo kutochanganya masuala hayo mawili kwa wakati mmoja, badala yake akawataka watambue kuwa kila suala lina wakati na umuhimu wake.
“Kuundwa kwa Kamati ya Pamoja ya Maridhiano yenye Wajumbe toka CCMZ na ACT ni suala la Kisiasa. Vyama hivyo vikumbuke ndivyo vyenye dhamana na wajibu wa kisheria na kikatiba hivyo hivina hiari,” alisema Mbeto.
Aidha, alisema Vyama hivyo vinapokuwa pamoja Serikalini ni rahisi kwao kukumbushana kuhusu utekelezaji wa hatua za kiutendaji za Kamati ya pamoja, kuliko chama kimoja kimo Serikalini na kingine kimetoroka.
“Sioni kama kuna tatizo. Kama lipo liko wapi hadi ACT kianze kusuasua. Kila kitu kiko wazi lakini wenzetu wanataka kujenga taharuki kwa wananchi ionekane kuna mjadala mkubwa bila kujali maslahi ya nchi,” alieleza.
Makubaliano na hatua za utekelezaji wake ni mchakato usiohitaji shinikizo lolote, ndiyo maana hakuna muda mahsusi toka hatua moja hadi nyigin, badala yake kila kitu kimewekwa kwa mpangilio na uwazi zaidi.
“ACT wasipoteze muda bure. Wasiwatie hofu wananchi kana kwamba kuna jambo kubwa mno losilowezekana. Kila kitu chini ya jua kinawezekana. Ndovu hajawahi kushindwa kubeba mkonga wake,” alisisitiza Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi alisema, pamoja na mbio zote za kisiasa, bado wananchi wanahitaji kupata huduma muhimu na maisha bora yanayotokana na utendaji wa shughuli za kisera za Serikali.
“Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi ndiye mwenye dhamana ya kuteua Kamati ya pamoja ya utekelezaji wa ajenda za Maridhiano. Tunamtaka Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Othman Masoud aache pupa na wahka. Zanzibar imepitia mengi na yote yamepita kwa salama,”alikumbusha Mbeto.