MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeendelea kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) katika kuendeleza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kufanya tafiti, kutoa ufadhili wa masomo na kuanzisha Redio Mtandaoni ya UDOM.
Akizungumza katika ofisi za UCSAF jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mulembwa Munaku, amesema Mfuko utaendelea kushirikiana na UDOM katika maeneo yenye manufaa kwa jamii na taifa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Redio Mtandaoni ya UDOM inaanza kufanya kazi na kuendeleza ufadhili kwa wanafunzi wanaosomea TEHAMA na Uhandisi.
Amesema ushirikiano huo pia utahusisha tafiti zitakazoiwezesha UCSAF kujitathmini, kuboresha huduma na kupata suluhisho zinazokidhi mahitaji ya wananchi, hususan katika matumizi ya TEHAMA na upatikanaji wa huduma za mawasiliano.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa UDOM, Prof. Lughano Kusiluka, ameipongeza UCSAF kwa ushirikiano wake, ikiwa ni pamoja na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa TEHAMA na Uhandisi, pamoja na kusaidia uanzishaji wa Redio Mtandaoni ya UDOM.
Prof. Kusiluka amesema UDOM, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inaendelea kuboresha miundombinu ya TEHAMA ili kuimarisha mazingira ya kujifunzia, kufundishia na kufanya tafiti, na kuongeza uwezo wa chuo kuvutia wanafunzi na watafiti kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Ushirikiano huo ni sehemu ya jitihada za kuendeleza matumizi ya TEHAMA, kukuza tafiti na ubunifu, pamoja na kuwawezesha vijana kupata elimu, ujuzi na fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia.