WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameiagiza Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) kuzifunga mara moja bucha zinazouza kiholela nyama na mazao yake bila kuzingatia sheria na kueleza kwamba hali hiyo inaweza kuathiri afya ya walaji.
Balozi Dkt. Bashiru amesema hayo Julai 27, 2026 baada kuelezwa kuwepo kwa changamoto hiyo kutoka kwa wachinjaji wa mifugo katika machijio ya Vingunguti yaliyopo Halmashauri ya Jijini Dar es Salaam.
Amesema kumekuwa na baadhi ya watu wamekuwa wakichinja wa mifugo hususan mbuzi na Kondoo kiholela hali inayorudisha nyuma jitihada za serikali ambayo imewekeza Shilingi Bilioni 19.5 kwa ajili ya ujenzi wa machinjio hayo ya kisasa.
“Kuna uuzaji holela wa nyama na mazao yake, kila mmoja amekuwa na machinjio yake (machinjio bubu), Bodi ya Nyama kamateni wote ambao wanamabucha ambayo hayajasajiliwa na ni bubu, wanaochinja barabarani, wanaochinja kiholela ni marufuku kwa sababu lazima uthibitishwe kuuza chakula hasa nyama, samaki na maziwa” amesema Dkt. Bashiru.
Balozi Dkt. Bashiru aliongeza kwa kuwahimiza viongozi wa halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuharakisha mchakato wa kupata wawekezaji kwa ajili ya kuendesha machinjio hayo kwa kukidhi taratibu na vigenzo vinavyokubaliwa na serikali vinginevyo machinjio hayo itafungwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar ea Salaam, Albert Chalamila amesema uendeshaji wa machinjio hayo unapaswa kuwa shirikishi kuanzia wizara za kisekta na kutafuta njia nzuri ya kuendesha machinjio ili kuleta tija iliyokusudiwa na serikali.
Awali, akisoma taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Dar es Salaam, Meneja wa Machinjio ya Vingunguti Dkt. James Kawamala alisema katika mwaka 2025/2026 mapato yaliyokusanywa kutokana na machinjio hiyo ni Shilingi Bilioni 2.075 sawa asilimia 90.02 ya lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 2.3 kutokana na uchinjaji wa mifugo ambapo takriban ng’ombe 500, mbuzi na kondoo 1,000 huchinjwa kwa siku.