Na WAF-Mtwara
WANANCHI kati ya 600 na 650 kutoka mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma wamepatiwa huduma mbalimbali za kibingwa na bingwa bobezi, ikiwemo upasuaji katika Kambi ya Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi inayoendelea kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini -Mtwara.
Kambi hiyo ni mwendelezo wa kambi za upasuaji zinazoandaliwa na Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini kwa lengo la kuwafikishia wananchi huduma za kwenye maeneo yao.
Akiongea wakati wa kutembelea kambi hiyo Julai 22 ,2026 Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, CPA Bahati Geuza, amesema Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 15.8 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, ikiwemo zaidi ya Shilingi Bilioni 9 kwa ajili ya vifaa tiba.
“Uwekezaji huu umeongeza uwezo wa hospitali hii ya Rufaa Kanda ya Mtwara kutoa huduma za kibingwa na Ubingwa bobezi kwa wananchi” amesema CPA Bahati
Kwa upande wake, Daktari Godfrey Sama, Mratibu wa Utafiti kutoka ECSA-HC, amesema kambi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu wa jumuiya hiyo kwa kuwafikishia wananchi huduma za afya, leengo ikiwa kuhakikisha tunawafikia wananchi na kutoa huduma kwa mgonjwa mmoja mmoja,” akibainisha huo ni mwendelezo wa kambi zilizowahi kufanyika katika nchi za Uganda na Lesotho.
CPA Bahati Geuza ametumia nafasi hiyo kuishukuru Wizara ya Afya, ECSA-HC pamoja na taasisi mbalimbali kwa kuratibu kambi hiyo, huku akiwataka wananchi wa Mtwara, Lindi na Ruvuma kujitokeza kupata huduma, ambazo zinaendelea kutolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mtwara.