SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaendelea kuimarisha juhudi za kuhakikisha kuwa masuala ya uendelevu wa mazingira yanapewa kipaumbele katika ajenda ya maendeleo ya Taifa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, aliposhiriki matembezi yaliyolenga kuhamashisha jamii katika Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira ‘Save Soil Walkathon’ yaliyofanyika Julai 19, 2026 jijini Dar es Salaam.
Masauni amesema, ahadi hii inaonyeshwa wazi katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2050, haswa nguzo yake ya Tatu, ambayo inatambua uendelevu wa mazingira na ustahimilivu wa hali ya hewa kama misingi muhimu wa kufikia mabadiliko ya kiuchumi jumuishi ya kijani kibichi na endelevu.
Ameongeza kuwa afya ya udongo ni msingi wa usalama wa chakula, uhifadhi wa mazingira na ustawi wa uchumi wa taifa, hivyo kuna umuhimu wa kila Mtanzania kushiriki katika juhudi za kuutunza.
“Udongo ni rasilimali muhimu inayobeba maisha yetu ya kila siku. Bila udongo wenye afya hatuwezi kuwa na usalama wa chakula, mazingira bora wala maendeleo endelevu. Ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki katika juhudi za kulinda mazingira na kutumia ardhi kwa njia zinazohifadhi uhai wake kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Masauni.
“Tunapoanza kutekeleza Mpango huu wenye kuleta mabadiliko makubwa, tunaona fursa nyingi za kuimarisha ushirikiano wetu na Jamhuri ya India. Tunatarajia kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali kama vile uhamishaji wa teknolojia, utafiti na uvumbuzi, ujenzi wa uwezo, urejeshaji endelevu wa ardhi, ufuatiliaji wa mazingira, uwekezaji rafiki kwa mazingira na suluhisho zinazozingatia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesisitiza Masauni.