MKUU wa Wilaya ya Iramba, Alhaj Suleiman Yusuph Mwenda, wiki hii Julai 16, 2026, amefanya ziara ya kukagua miradi itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru 2026 pamoja na kujionea maandalizi ya mapokezi ya Mwenge huo wilayani humo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Alhaj Mwenda amewapongeza watumishi, wananchi wa Wilaya ya Iramba na Halmashauri kwa maandalizi mazuri ya kuupokea Mwenge wa Uhuru. Amesema maandalizi hayo yanaonesha utayari wa Wilaya ya Iramba kuupokea na kuukimbiza Mwenge wa Uhuru kwa mafanikio makubwa.
Aidha, amewahimiza wananchi wote wa Wilaya ya Iramba kujitokeza kwa wingi Julai 24, 2026 kuupokea na kushiriki mbio za Mwenge wa Uhuru, akieleza kuwa tukio hilo ni fursa ya kuendelea kuhamasisha uzalendo, umoja, maendeleo na ushiriki wa wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kwa mujibu wa ratiba, Mwenge wa Uhuru 2026 utapokelewa katika Uwanja wa Mcharukoni, Kijiji cha Ndulungu, huku mkesha wa Mwenge ukifanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Misigiri.