Na Albert Kawogo
BAADHI ya wanachama na makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wameonyesha kusikitishwa na mwenendo wa sasa wa Chama hicho hususan kwenye maeneo ya uadilifu na uwajibikaji, huku lawama kubwa wakizielekeza kwa Makamu Mwenyekiti John Heche na Katibu John Mnyika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanachama hao wamesikitishwa na mwenendo viongozi hao kuikataa hoja ya maridhiano huku wakiweka shinikizo kwa serikali kumtoa mahabusu Mwenyekiti wao Tundu Antipas Lissu wakiita huko ni kuiingilia uhuru wa mahakama
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano na aliyewahi kuwa mwanachama wa CHADEMA, Odero Charz Odero, ametoa wito kwa Viongozi wa Chama chake kurekebisha kauli zao hasa wanapokuwa wanalenga Serikali na hata kumuhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan na suala la Tundu Lissu.
“Rais hapewi amri ili avuruge uhuru wa mhimili mwingine akifanya hivyo anavunja katiba sasa naomba viongozi wangu watambue hii nchi inaendwa chini ya mwamvuli wa katiba na Rais anaapa kuilinda,” amesema Odero.
Odero amesema, nchi inahitaji kuingia kwenye maridhiano na kauli za viongozi wetu ziwe za kujenga daraja la mazungumzo ili muafaka wa kitaifa upatikane.
Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Morogoro Barnabas Okola amesema, Mwezi Septemba 2025, chama chao kiligoma kusaini kanuni za uchaguzi Mkuu wa 2025 matokeo kikapoteza haki ya kusimamisha wagombea kwenye ngazi zote na hivyo kuwanyima wanachama wote haki ya kuchaguliwa na sasa wanataka tena kupoteza fursa ya kuingia kwenye maridhiano
“Viongozi wetu wanatukatisha tamaa sana,tulipoteza fursa ya kugombea na sasa wanataka kukataa kuingia kwenye maridhiano naiona hii ni fursa nyingine tunataka kuipoteza sioni mantiki kwenye jambo hili,” amesema Okola.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHADEMA wa Wilaya ya Mwanga na mjumbe wa Baraza Kuu Taifa Lembrus Mchome amesema, suala la maridhiano na tuhuma za ufisadi za Makamu Mwenyekiti John Heche zimefanya wanachama wanaonyesha msimamo kuandamwa na kufukuzwa kwenye chama.
Mchome amesema, CHADEMA si mali ya mtu ni taasisi ya umma inayosimamiwa na kikatiba hivyo kiongozi yeyote anaekwenda kinyume na Katiba ya taasisi lazima awajibishwe.
“Mtu ukitoa maoni yako siku haiishi unafukuzwa ,tutapoteza watu wengi sasa hii demokrasia tunajinasibu nayo kwenye chama chetu ni ipi? Anauliza Mchome.
“Hatuwezi kuwa na viongozi wanaohubiri uadilifu huku wao sio waadilifu huku ni kukiua Chama na kusaliti misingi ya uanzishwaji wake,namuomba Makamu wangu Mungu ampe maono ya kujitafakari sana,” amesema.
Issa Mwinamila kada maarufu wa CHADEMA mkoani Tabora amepeleka lawama kwa Katibu Mkuu kwa kuongea kauli za kukatisha wanachama pale alipoonyesha kumlinda wazi wazi Makamu Mwenyekiti John Heche kwenye tuhuma za kupokea fedha kwa niaba ya Chama na kuzitumia
Mwinamila ameongeza kwa kusema, chama chao kilishaikamata CCM kwenye maeneo mengi nchini kutokana na mikutano yao kujaa watu, ila tuhuma za Heche zimewarudisha nyuma na kupunguza imani za Watanzania.