Na Mwandishi Maalum, Arusha
MBUNGE wa Arusha Mjini na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda amewataka madaktari, wauguzi, wataalamu wa maabara na watumishi wote wa afya watakaoshiriki Kambi ya Matibabu Bila Malipo Arusha kutoa huduma kwa huruma, upendo na utu, ili kila mwananchi anayefika apate matumaini mapya ya maisha.
Akizungumza na timu ya madaktari na wataalamu wa afya kabla ya kuanza kwa kambi hiyo, Makonda amesema huduma wanazokwenda kuzitoa si kazi ya kawaida pekee, bali ni huduma yenye thamani kubwa mbele za Mungu kwa kuwagusa watu wanaopitia changamoto mbalimbali za kiafya na kiuchumi.
“Mtakutana na watu waliopoteza matumaini, wenye magonjwa ya muda mrefu na wengine wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu. Hakikisheni kila anayepita mikononi mwenu anaondoka akisema, ‘Mungu asante’,” amesema Makonda.
Amesisitiza umuhimu wa kuwahudumia wagonjwa kwa uvumilivu, kuwapa muda wa kueleza changamoto zao na kuwatendea kwa heshima bila kujali hali zao za maisha.
Aidha, amewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na madaktari, hospitali, taasisi na wadau wote waliojitokeza kuunga mkono kambi hiyo ya matibabu, akieleza kuwa ushirikiano huo unawapa maelfu ya wananchi fursa ya kupata huduma za kibingwa bila malipo.
Kambi hiyo ya matibabu itafanyika kuanzia Julai 13 hadi Julai 19, 2026 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, ambapo madaktari bingwa kutoka hospitali mbalimbali nchini watatoa huduma za uchunguzi na matibabu katika fani mbalimbali za kibingwa.