Na Albert Kawogo, Zanzibar
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema uungwana haupaswi kuzaa kiburi wala kutoweka nafasi ya kusikilizana, akisisitiza kuwa matarajio makubwa ya wananchi ni kuona nchi ikiendelea kuwa na amani, utulivu na mshikamano.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Julai 9,2026 alipohudhuria hafla ya kushuhudia utiaji saini wa Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa kati ya vyama vya siasa Zanzibar, iliyofanyika katika Ikulu ya Zanzibar.
Amesema, maridhiano sio unyonge bali ni mazungumzo yenye kuheshimiana na pia ni msingi muhimu wa kujenga taifa lenye umoja na maendeleo, huku akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuweka mbele maslahi ya wananchi badala ya tofauti zao za kisiasa.
Kauli ya Rais Samia imekuja katika hafla inayotajwa kuwa hatua muhimu ya kuimarisha maelewano ya kisiasa na kudumisha amani nchini, hususan Zanzibar
Kwa upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi, amesema kusainiwa kwa Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa Zanzibar ni hatua ya kihistoria yenye umuhimu mkubwa katika kuimarisha amani, mshikamano na ustawi wa wananchi wa Zanzibar na taifa kwa ujumla.
Dkt. Mwinyi amesema ushirikiano kati ya viongozi na wananchi ni msingi wa kuleta maendeleo endelevu huku akiwahimiza wananchi na viongozi kuendelea kushirikiana katika kulinda mafanikio ya maridhiano hayo.
Rais huyo wa Zanzibar ameeleza kuwa Serikali itaendelea na awamu ya pili ya utekelezaji wa mchakato huo kupitia ajenda zilizokubaliwa na pande zote mbili nia ikiwa ni kuepuka makosa yaliyowahi kufanyika kwenye maridhiano yaliyowahi kufanyika huko nyuma.
Aidha, amesema hatua zote zilizofanyika kwenye mchakato huo zimelenga kuimarisha umoja, utulivu na maendeleo ya Zanzibar
Awali, akizungumza kwenye hafla hiyo Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Othman Masoud Othman alisema uamuzi wa kuingia katika maridhiano ya kisiasa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar umetanguliza maslahi ya wananchi.
“Kukiwa na giza tunahitaji mwanga, hatuwezi kuruhusu giza liendelee lazima tuwashe taa,na taa yetu ni mazungumzo yaliyozaa tamko hili yeyote anaepinga tamko hili haitakii mema Zanzibar,” amesema Masoud.