KAMANDA wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ( SACP) Jumanne Muliro, ametembelea banda la Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo alipokea maelezo kuhusu utekelezaji wa miradi ya mawasiliano inayosimamiwa na UCSAF nchini.
Akiwa katika banda hilo, Kamanda Muliro alifahamishwa kuhusu juhudi za UCSAF katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano, hususan katika maeneo ya vijijini na yasiyo na mvuto wa kibiashara.
Pia, alijionea mafanikio ya miradi inayotekelezwa na UCSAF katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma za simu na intaneti, hatua inayochangia kuimarika kwa ulinzi na usalama pamoja na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Ziara hiyo imekuwa sehemu ya shughuli zinazoendelea katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo UCSAF inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu miradi yake na mchango wake katika kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia Watanzania wengi zaidi.