Na Albert Kawogo
AfrikaLEO Online
UNAWEZA ukajiuliza na kisha ukajibu kuwa, ni kweli kwamba Namibia si miongoni mwa washirika wakubwa wa biashara wa Tanzania kwa kuzingatia kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili.
Takwimu za mwaka 2024 zinaonesha kuwa Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Dola Milioni 2.38 kwenda Namibia, huku Namibia ikiuza bidhaa za thamani ya Dola Milioni 5.96 kwenda Tanzania.
Kwa mtazamo wa kawaida, kiwango hiki ni kidogo ikilinganishwa na biashara ya Tanzania na nchi kama China, India, Kenya au Afrika Kusini na baadhi ya nchi za Ulaya
Hata hivyo, diplomasia ya kisasa haijengwi kwa kuangalia biashara ya leo pekee, bali pia fursa za kesho, usalama wa kikanda, historia ya mahusiano na maslahi ya kimkakati ya muda mrefu.
Ni vema kwa ikumbukwe kuwa Tanzania na Namibia zina historia ya kipekee ya ukombozi wa Afrika. Tanzania iliunga mkono harakati za ukombozi wa Namibia kupitia chama cha SWAPO wakati wa mapambano dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini.
Uhusiano huu wa kihistoria umeendelea kuwa msingi wa ushirikiano wa kisiasa kati ya mataifa hayo mawili.
Lakini, kingine ni kwamba Namibia ni moja ya nchi zenye utajiri mkubwa wa madini muhimu duniani, ikiwemo uranium, almasi na madini yanayotumika katika teknolojia za kisasa.
Tanzania inaweza kunufaika kwa kushirikiana na Namibia katika kubadilishana uzoefu wa usimamizi wa rasilimali za madini na kuvutia uwekezaji.
Tunaangazia fursa nyingine ni kwamba,marais wa Tanzania na Namibia wamekuwa wakitafuta kuongeza biashara ambayo kwa sasa bado iko chini. Ziara za viongozi mara nyingi huwa chachu ya kufungua masoko mapya, kuondoa vikwazo vya biashara na kuhamasisha sekta binafsi kushirikiana zaidi.
Namibia ina bandari muhimu ya Walvis Bay inayounganisha nchi za Kusini mwa Afrika na masoko ya Kimataifa.
Ushirikiano kati ya Dar es Salaam na Walvis Bay unaweza kuimarisha biashara ya kikanda na usafirishaji wa bidhaa ndani ya Afrika chini ya Mpango wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Kwa hiyo, swali si “Namibia ina biashara kubwa kiasi gani na Tanzania leo?” bali “Namibia inaweza kuwa mshirika wa kimkakati kwa Tanzania katika miaka ijayo?” Kwa viongozi wa nchi hizi mbili, jibu linaonekana kuwa ndiyo.
Ndio maana tunaona ziara za mara kwa mara, mikutano ya ngazi za juu na msisitizo wa kuimarisha ushirikiano licha ya kiwango cha sasa cha biashara kuwa bado ni kidogo.
Kwa kifupi, Tanzania inaiona Namibia kama mshirika wa kimkakati wa muda mrefu katika diplomasia, uwekezaji, madini, usafirishaji na ushirikiano wa kikanda, si kwa sababu ya ukubwa wa biashara ya sasa pekee.