Na Clements Robert, WAF
WIZARA ya Afya imesema jumla ya tetesi 64 za ugonjwa wa Ebola kutoka mikoa 21 nchini zimechunguzwa tangu kutangazwa kwa tishio la ugonjwa huo katika nchi jirani na hakuna aliyebainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo mpaka sasa.
Akizungumza jijini Dodoma Juni 18, 2026, wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa Ebola, Waziri wa Afya, Mohamed Omary Mchengerwa, amesema mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa imeendelea kufanya kazi kwa ufanisi katika kubaini na kuchunguza kwa haraka visa vinavyotiliwa shaka.
“Mpaka sasa tetesi 64 kutoka mikoa 21 zimeripotiwa, kati ya hizo wahisiwa 11 walikidhi vigezo vya uchunguzi, wakachukuliwa sampuli na baada ya kupimwa walithibitika kutokuwa na maambukizi ya Ebola,” alisema Mchengerwa.
Amesema Serikali imeendelea kuimarisha ufuatiliaji wa tetesi katika jamii, vituo vya kutolea huduma za afya na maeneo ya mipakani ili kuhakikisha viashiria vyovyote vya ugonjwa huo vinagunduliwa mapema na kuchukuliwa hatua stahiki.
Kwa mujibu wa Waziri Mchengerwa, wataalam wa afya nchini wameendelea kupatiwa miongozo, vifaa kinga na vitendea kazi vinavyohitajika ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa usalama na ufanisi katika kipindi hiki cha tahadhari.
“Matokeo haya yanaonesha kuwa mifumo yetu ya ufuatiliaji na uchunguzi wa magonjwa inaendelea kufanya kazi vizuri, lakini bado tunapaswa kuendelea kuwa makini kutokana na uwepo wa mlipuko katika nchi jirani,” alisema.
Waziri Mchengerwa pia amewahimiza wananchi kutoa taarifa mapema kwa wataalam wa afya wanapoona dalili au viashiria vinavyoweza kuashiria uwepo wa ugonjwa huo ili hatua za uchunguzi ziweze kuchukuliwa kwa wakati.