Na Hamis Shimye
BAJETI ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27 iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, imepokelewa kwa pongezi mbalimbali kutokana na na mwelekeo thabiti wa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi.
Bajeti hiyo yenye thamani ya Shilingi Trilioni 62.33 inaonesha ongezeko linaloashiria kuimarika kwa uwezo wa Serikali katika kugharamia miradi ya maendeleo na huduma za kijamii.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za kuendeleza mageuzi ya kiuchumi yanayolenga kujenga uchumi imara na shindani zaidi.
Wachambuzi wa masuala ya uchumi wameipongeza Serikali kwa msisitizo wake wa kuongeza mapato ya ndani, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa mikopo na misaada ya nje.
Mkakati huo unatajwa kuwa msingi muhimu katika kuimarisha uhuru wa kifedha wa taifa na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa bajeti hasa eneo la uchumi wa kidijitali.
Aidha, kipaumbele kilichotolewa kwa miradi ya kimkakati kama reli ya kisasa (SGR), miundombinu ya barabara, nishati, maji, elimu na afya kimeelezwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi na upatikanaji wa ajira kwa wananchi, hususan vijana.
Serikali pia imeendelea kusisitiza usimamizi madhubuti wa uchumi kwa kuhakikisha uthabiti wa bei, kuimarisha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Kwa ujumla, Bajeti ya 2026/27 imeelezwa kuweka msingi imara wa kufanikisha malengo ya maendeleo ya muda mrefu, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku ikijenga matumaini mapya ya ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.
Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar pamoja na watendaji wote wa Wizara, hongereni kwa kutuletea bajeti nzuri na ya kipekee na yenye mwelekeo chanya na wa kimkakati kwa mustakabali wa maendeleo ya Tanzania. Mungu ibariki Tanzania..