RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji, uwazi na sera rafiki ili kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha uwekezaji kinachotambulika katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Juni 10, 2026, aliposhiriki dhifa maalum ya Singapore–Zanzibar Business Networking Dinner iliyofanyika Fumba, Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Singapore kutumia fursa zilizopo Zanzibar katika sekta za utalii, uchumi wa buluu, biashara, teknolojia, huduma na miundombinu.
Amesema ziara ya Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, pamoja na Jukwaa la Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Zanzibar na Singapore, zimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi na uwekezaji kati ya pande hizo mbili.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ametunukiwa Tuzo Maalum ya Uongozi katika Uwekezaji na Shirikisho la Wawekezaji la Singapore kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuvutia mitaji Zanzibar.
Dhifa hiyo ya chakula cha usiku imewajumuisha viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Singapore na Zanzibar, pamoja na wadau wa sekta ya uwekezaji kutoka sekta binafsi.