WANACHAMA wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kujiepusha na siasa za kuchafuana wakati huu wa kuelekea kwenye chaguzi za kuwania nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho tawala na Uchaguzi Mkuu 2030.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto amesema, chama hicho kina demokrasia kubwa, hivyo muda ukifika kila mmoja atakuwa na haki ya kumuunga mkono mgombea anayeona anafaa, kwahiyo hakuna haja ya kuchafuana.
“Tunaelekea karibu na uchaguzi wa chama, kutakuwa na nafasi za urais huko mbele, watu watataka kuchafuana, watu watataka kutengeneza makundi na kambi zao, lakini chama chetu kina demokrasia kubwa, ukifika wakati kila mtu ana haki ya kumuunga mkono mgombea anayeona anafaa, hakuna haja ya kuwachafua watu ambao wametengeneza heshima kubwa kwa nchi yetu, wameaminika,” alisema Mbeto.
Alisema, licha ya madai yanayotolewa kuhusu baadhi ya wateule, lakini chama hakijapokea taarifa yoyote kama kuna tatizo ndani ya Serikali zote mbili; Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
“Wote (wateule) wanafanya kazi vizuri na kila kiongozi anatumwa na Kiongozi Mkuu wa nchi kwenda kumwakilisha na pale anapotumwa anatekeleza majukumu yake na anaweka wazi amekwenda kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar, kwahiyo tuache hisia zetu na misukumo,” alisisitiza Mbeto.
Aidha, Mbeto alisema wanachama na viongozi wa CCM wanapaswa kuwa makini kipindi cha kuelekea kwenye chaguzi za chama, “tutaona mengi huko tunapokwenda, ila chama chetu kipo makini, kinaangalia kila hatua, kila sauti. Kinaangalia kila maelezo, kikigundua tofauti chama kitawaita,”
“Maana ni makada wetu, muda wote wanaweza kuitwa kututhibitishia tuhuma dhidi ya viongozi wetu wakuu akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya wateule wao na chama kitachukua hatua, viongozi wetu nao wana hatua wanaweza kuchukua.”