Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepongeza uamuzi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Rais Dkt. Hussein Ali Mwimyi kwa kushinda majaribu ya wapambe walioanza kumshinikiza avunje katiba na kuongeza muda wa kubaki Madarakani Zanzibar.
CCM kimesema, ni fedheha kwa wapambe na mashabiki walioanza kumshawishi kiongozi huyo abaki madarakani kinyume na Katiba ya CCM na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, aliyesema huo ndio uamuzi na msimamo wa CCM.
Mbeto alisema, kwa mujibu wa Mila na Utamaduni wa CCM, na kwa matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na katiba ya CCM, Rais atakaa Madarakani vipindi viwili vya Miaka kumi na hatawania tena nafasi hiyo.
Alisema, matamshi yaliyotamkwa na baadhi ya wapambe kwa utashi wao binafsi, yalikuwa na dhamira batili, kwani hakuna Rais kupitia CCM anayeweza kupata nafasi ya kuongeza muda wa kubaki madarakani kinyume na taratibu.
“Hata iweje kwa Rais aliye Madarakani akitokea ameleta maajabu ya kiutendaji katika kusimamia maendeleo, muda wake kikatiba utabaki kuwa ule ule wa miaka kumi madarakani. Kila Rais akimaliza miaka hiyo atawapisha wengine.” alisema Mbeto.
Aidha, Katibu huyo Mwenezi aliliita tangazo la Rais Dkt. Mwinyi kukataa kubaki ikulu ifikapo mwaka 2030, hana fikra wala mpango wa kuongeza muda ili abaki madarakani, ni aibu kwa walioanza kumshabikia.
“Kiongozi yeyote muungwana huheshimu l aidha yla chama na Katiba ya nchi. Kuvunja ahadi na miadi au kufanya kinyume chake hiyo ni dalili ya kiongozi huyo kukosa utu na ustaarabu” alisisitiza.
Mbeto alisema Tanzania hususan ndani ya CCM, kuna wanachama wengi wenye uwezo wa kubeba dhamana ya Urais na kuitumikia nchi kwa uzalendo, uadilifu na uaminifu, hivyo nafasi ya kiongozi mmoja kubaki madarakani milele haipo.
“Nafasi zaidi ya miaka mitano ilitolewa kwa Waasisi Wetu Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume. Baada ya wao hatatokea yeyote wa kuongeza muda zaidi ya kuongoza aidha kwa Zanzibar au Tanzania,” alieleza Mwenezi huyo.