Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimewataka Viongozi Wastaafu, Wanataaluma, Wasomi Wabobezi na Wachambuzi wa Masuala ya Kisiasa, Kijamii na Kiuchumi, kutambua dhima ya gharama ya kujenga Taifa ni ghali kuliko hasara ya kulibomoa.
Pia, kimetaja ulimi wa binadamu unapototoa maneno bila tafakuri ni sawa na kuchezea upanga wenye makali au kuwasha moto unaosambaa na kuteketeteza Misitu, Mbuga na Nyika.
Maneno hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyewataka Watanzania kujua thamani ya Umoja wao kuliko hasara ya kutoa maneno yanayopandikiza chuki, hasama na upasi katika jamii.
Mbeto alisema wananchi, wastaafu, wasomi, wachambuzi na wanataaluma wanaopaswa kuwa wa kwanza kuitakia mema Tanzania na kwamba hata watakaolifikisha miaka sitini ijayo huku Taifa likiwa moja ni Watanzania wenyewe.
Akizungumza bila kutaja majina ya watu, vyeo au Taasisi zao, Mbeto alisema hivi karibuni kumezuka tabia ya baadhi ya watu kutamka maneno bila kupima athari na faida zake katika jamii yenye watu waungwana .
“Tabia ya baadhi ya viongozi Wastaafu kutoa maneno makali bila kuyapima ni hatari . Pia kuna baadhi ya Wasomi na Wanataaluma wanaoheshimika hutamka maneno ya kuogofya. Wajue tu maneno makali hubomoa badala ya kujenga nchi,” alisema Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi alisema ipo haja ya kujadiliana mambo kwa kufuata taratibu zinazofaa ambazo haziachi athari katika jamii lakini pia si uungwana watu wazima wakawa na sifa ya kusemasema hovyo kila uchao ili kutaka sifa ya utukufu.
“Ni kosa mtu kufikiri yatakapozuka majanga au machafuko ana uhakika wa kubaki salama. Fujo, ghasia na vurugu hazina macho wala masikio. Huwadhuru matajiri, masikini, viongozi na raia wema wasio na hatia bila kutarajia,” alisema.
Aidha, Katibu Mwenezi huyo alisema hakuna gumu lisiloweza kuzungumzika na kumalizwa kwa njia za kiungwana , hivyo aliwashauri viongozi wastaafu wa ngazi zote, Wanataaluma na Wasomi Wabobezi, maneno yao yajiegemeze zaidi katika kujenga na kulinda umoja wa Kitaifa.
“Wapo baadhi ya wenzetu wanataka kutumia fujo na vurugu kama mtaji wa kushika madaraka. Huwezi kupata utawala kwa mbinu hizo batili. Njia pekee inayokubalika ni demokrasia ya uchaguzi ili kushika uongozi badala ya kususia,” alikumbusha Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi alisema kuna baadhi ya wanasiasa wanapohutubia kwenye majukwaa mbele ya wananchi, hawataki kuzingatia mantiki ya kisheria inavyosema badala yake huvuka mipaka huku wakitamka na kueneza shari.
“Siasa za kuhubiri shari zimeyavuruga Mataifa mengi hususan Barani Afrika. Maneno makali yasio na vipimo yamevuruga umoja, Amani na kusibabisha mauaji, Vita na Umwagaji damu,” alisisitiza Mbeto.