Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis
Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesema kipo tayari kuyafanyia kazi maagizo manne ambayo yametolewa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi wakati wa ziara yake aliyoifanya hivi karibuni.
Chama hicho kimesema, ziara hiyo ambayo ilianza Mei 9, 2026 ni mahsusi kwa ajili ya kuwashukuru wanachama na viongozi waliohakikisha chama chao kinashinda kwa asilimia 75, kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa ziara hiyo.
Mbeto alisema, licha ya kuchelewa kwa ziara hiyo kutokana na changamoto ambazo zilijitokeza bara baada ya uchaguzi, lakini imekuwa na mafanikio makubwa na mwitikio umekuwa mkubwa.
Alisema, wakati wa mikutano yake aliyoifanya kwenye mikoa yote ya Unguja na Pemba, Makamu Mwenyekiti Dkt. Mwinyi alisisitizia maazimio manne ya Halmashauri Kuu Taifa ambayo ni chama kujifanyia tathimini, chama kuwa na uwezo kiuchumi, kusimamia maadili na kufanya mafunzo kwa makada wake.
“Ziara imekuwa nzuri, mwitikio ni mkubwa, tuna imani yale yote ambayo ameyasema Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti kama chama, tutakwenda kuyafanyia kazi, lakini jingine anataka kukiona chama kimeimarika na anataka vile viungo vyote vya chama, kwa maana ya Kamati zote za chama zinafanya kazi vizuri,” alisema Mbeto.
Aidha, Mwenezi huyo alisema Makamu Mwenyekiti aliwaasa wanachama wa CCM kuhakikisha wanajiepusha na Makundi wakati huu wanapoelekea kwenye chaguzi za ndani ya chama.
“Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti aliwaasa wabunge na wawakilishi waache makundi, waendelee kutekeleza ilani, wasiwabague wanachama wao,” alisisitiza Mbeto.