📌Asema mapambano dhidi ya uhalifu yanahitaji mshikamano wa kimataifa
📌Aeleza teknolojia ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na uhalifu wa kisasa
WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema ushirikiano wa kikanda na kimataifa ni sharti la mafanikio katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa unaozidi kubadilika na kuvuka mipaka.
Amesema kuwa katika dunia ya sasa, aina nyingi za uhalifu hupangwa, hufadhiliwa na kuratibiwa kwa njia za kidijitali, hali inayohitaji mifumo imara ya kiteknolojia pamoja na ushirikiano wa pamoja ili kuudhibiti kwa ufanisi.
Ametoa kauli hiyo Mei 4, 2026, wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa 11 na Kongamano la Chama cha Waendesha Mashtaka Afrika Mashariki (EAAP), unaofanyika katika Ukumbi wa Blue Sapphire, jijini Dar es Salaam, kuanzia tarehe 4 hadi 6 Mei, 2026, wenye
“Kama ambavyo uhalifu uliopangwa hauwezi kuwepo bila kuvuka mipaka, vivyo hivyo vyombo vya dola na mifumo ya haki ya jinai haviwezi kukabiliana nao kwa ufanisi bila kuwa na mifumo madhubuti ya ushirikiano wa kimataifa, hususan katika maeneo ya msaada wa kisheria na urejeshaji wa watuhumiwa,” alisema.
“Utafiti unaonesha kuwa katika hali nyingi, uhalifu dhidi ya wanyamapori na uhalifu wa kimataifa hupangwa kidijitali, hufadhiliwa kwa njia za kielektroniki na kuratibiwa kuvuka mipaka, na pia hufichwa kwa kutumia mbinu tata za kiteknolojia, hali inayofanya mipango na athari zake kuvuka mipaka kwa kasi kubwa ambayo wakati mwingine hupita bila kugundulika.”
“Katika mazingira haya, hatuwezi kufanikiwa katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa uliopangwa bila kutumia kikamilifu teknolojia kama nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto hii ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla,” alisema.
“Ni dhahiri kwamba biashara haramu ya wanyamapori na aina nyingine za uhalifu wa kimataifa uliopangwa ni tishio kubwa kwa mataifa yetu; unachangia kupotea kwa rasilimali zetu na pia ni tishio kwa utulivu na usalama wa nchi zetu,” alisema.