HAZINA Sport Club imeendelea kufanya vizuri katika michezo mbalimbali hususani mpira wa pete ulioifanya kuingia nusu fainali dhidi ya timu ya Ikulu ikiwa ni sehemu ya michezo inayoendelea Mkoani Njombe kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani Meimosi 2026, ambapo Kitaifa itafanyika Mkoa wa Njombe.
Akizungumza baada ya mchezo kati ya Hazina na Ikulu, Kapteni wa Timu ya Hazina, Upendo Kavalambi alisema kuwa, walikuwa na mchezo mzuri katika hatua ya robo fainali kati ya Hazina dhidi ya Uchukuzi ambapo Hazina iliibuka kidedea kwa kuichapa Uchukuzi bao 41 kwa 35 na kusababisha Hazina kutinga Nusu Fainali dhidi ya Ikulu.
Kavalambi amesema kuwa Nusu Fainali wamemenyana na Timu ya Ikulu japo bahati haikuwa kwa upande wa Hazina lakini hatua ya kufika nusu fainali haikuwa rahisi kwa kuwa miaka kadhaa Hazina haikuwahi kufika hatua hiyo hasa kwa mpira wa pete.
Alisema kuwa michezo inasaidia kujenga umoja na mashirikiano kwa watumishi lakini pia kujenga afya inayoboresha utendaji mahali pa kazi.
Aidha, alisema kuwa Hazina Sport Club itaendelea kushiriki kikamilifu katika michezo hiyo na kwamba wataendelea kufanya vizuri siku za usoni kwa kuongeza kiwango cha mazoezi ya kiushindani ili kuwa bora zaidi.