RIPOTI ya Tume ya Jaji Othman Chande kuhusu matukio ya Oktoba 29, 2025 imesomwa na kuwasilishwa kwa Rais, lakini haipaswi kusomwa kama historia tu.
Ni kioo kinachotuonyesha tulipoponyoka au kuteleza kidogo kwa tamaa za fedha, uwakala na kutumiwa, siasa hasi, usaka madaraka, uhalifu na hali za kijamii na kiuchumi.
Ripoti iliyowasilishwa Alhamisi, Aprili 23, 2026, imeeleza wazi nchi yetu ilihanikizwa na vurugu zilizopangwa na watu waliodhamiria kuisukuma Tanzania kwenye ombwe la uongozi endapo uchaguzi usingefanyika.
Vijana waliohusika hawakuamka asubuhi na kuokota mawe barabarani bila utaratibu. Walikuwa wamejiandaa kufanya tukio siku hiyo. Walianza vurugu zao mwendo wa saa tano hadi sita wakati watu wakipiga kura. Lengo ni kuvuruga uchaguzi kama ilivyokuwa ikielekezwa kupitia akaunti maalum za mtandao ya kijamii.
Walikuwa na nondo, mishale, mapanga na bunduki, silaha zinazohitaji uratibu wa kifedha, kiusalama na mafunzo. Walivamia mali za wananchi, vituo vya mwendo kasi, maduka yalichomwa, magari yakateketezwa.
Walivamia vituo vya polisi, ofisi za chama cha CCM na Serikali za mitaa, kata na kuzichoma moto, pia wakavunja ATM za CRDB, NMB na NBC kupora fedha na kusababisha hasara inayokadiriwa kufika Shilingi Bilioni 36.
Kwa mujibu wa ripoti ya Tume, watu hao walijaribu kuzima mawasiliano ya baadhi ya mitambo ya serikali au kuzusha kuwa wanatia sumu maji. Walivamia biashara za watu binafsi na kusababisha hasara ya Bilioni 80 kwa mujibu wa Ripoti ya Tume.
Kitendo cha kulizidi jeshi la polisi katika maeneo matatu ya Dar es Salaam si dalili ya hasira ya ghafla, ni ushahidi kuwa walipitia mafunzo mazito ya mbinu za kivita, udanganyifu na uzushi wa kitaarifa (disinformation) na usambazaji wa haraka. Kama Tume ilivyosema, walikuwa na vituo vya siri vya mafunzo vilivyosambaa jijini Dar es Salaam na mikoani.
Tusijidanganye kuwa haitatokea kwetu kama hatutadhibiti haya mapema na kwa hatua munasibu. Mwaka 2011, Libya iliyokuwa na utulivu wa miaka 42 iliangushwa ndani ya miezi minane baada ya maandamano yaliyoanza kama malalamiko ya mitaani kugeuzwa vurugu za silaha. Mali za umma ziliteketezwa, vikosi vya ulinzi viligawanyika, na hadi leo Libya haina serikali moja imara.
Mwaka 2014, Ukraine ilipoteza amani baada ya makundi yenye mafunzo ya kijeshi kuchukua uwanja wa Maidan; matokeo yake ni vita vinavyoendelea hadi leo.
Syria 2011 kilichoitwa chemchemi ya Waarabu kiligeuka uwanja wa mauaji baada ya vikundi vyenye silaha kuizidi dola.
Katika yote hayo, mwanzo ulikuwa sawa na Oktoba 29 yetu, vijana waliojitokeza na hasira, walibeba silaha za hatari, na mpango wa kubemenda mamlaka ya dola.
Prof. Ted Robert Gurr, mwandishi wa ‘Why Men Rebel’ anaonya kuwa vurugu za kisiasa hupanda ngazi tatu: malalamiko, uhamasishaji, kisha vurugu za silaha.
Oktoba 29 ilikuwa ngazi ya tatu. Dkt. Marina Ottaway wa Carnegie Endowment anaeleza kuwa dola ikionekana dhaifu mbele ya makundi yenye silaha, hupoteza udhibiti wa vurufu (monopoly of violence) na hapo ndipo hupanda mzuka na kufanya mapinduzi au kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe. Tuvishukuru sana vyombo vyetu vya dola kwa mbinu na uzalendo viliyoonesha.
Kwa upande wa intelijensia, Bruce Hoffman wa Georgetown University anasema, matukio ya namna hii yakiachwa bila kuwawajibisha wahusika wakuu, yanakuwa chuo cha uhalifu, kizazi kijacho hujifunza kuwa vurugu ndiyo njia ya kupata unachokitaka.
Pendekezo la Tume kuunda Tume ya Maridhiano ni sahihi. Taifa linahitaji kupona. Lakini maridhiano hayawezi kuwa zulia la kufunika damu. Waliohusika na vurugu zile kwa nafasi zozote walizonazo katika jamii wawajibishwe.
Kama anavyosisitiza Prof. Mahmood Mamdani katika ‘When Victims Become Killers,’ msamaha bila ukweli na uwajibikaji ni mwaliko wa mauaji mengine.
Waliopanga, waliofadhili na waliofunza vijana hao Oktoba 29 si wazushi wa kisiasa ni wahalifu wa jinai. Ni lazima wakamatwe, wachunguzwe na wafikishwe mahakamani.
Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, inataaja wazi, kula njama za kutenda kosa la uhaini, kumiliki silaha kinyume cha sheria, na kuchochea uasi. Vyombo vya dola vikichelewa, vitakuwa vinatuma ujumbe mbaya kwamba Tanzania inaweza kuvurugwa na mtu akarudi nyumbani salama.
Oktoba 29 imetuonyesha kuwa adui wa amani yetu si hoja za kisiasa, bali vurugu mikononi mwa watu wasiowajibika. Dawa 12 za Jaji Chande ni nzuri matibabu, Katiba Mpya 2028, Tume ya Maridhiano.
Hata hivyo, dawa ya kwanza ni sheria. Serikali iunde mara moja Kikosi Maalum cha upelelezi, kwa ushirikiano wa TAKUKURU, Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa, kufuatilia mtandao mzima wa uhalifu huo.
Mahakama zisisite kuwahukumu wahalifu hadharani ili Taifa lijifunze. Maridhiano yajengwe juu ya jiwe la haki. La sivyo, tutakuwa tunapanda mbegu ya Oktoba 29 nyingine na wakati ujao, huenda tusiwe na bahati ya kuponyoka na kujinusuru.