Na Mwandishi Wetu, Arusha
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, jana Aprili 17, 2026 amekagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu unaojengwa mkoani Arusha kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya AFCON 2027.
Uwanja huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa miundombinu muhimu itakayotumika wakati wa mashindano hayo yatakayofanyika kwa pamoja katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Dkt. Nchemba amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya kimataifa, ili kuiwezesha Tanzania kuwa mwenyeji bora wa mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.
Amesema Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya kimkakati ili kuhakikisha nchi inanufaika kikamilifu na fursa zinazotokana na mashindano ya AFCON 2027.