RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema wakati umefika kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuangalia fursa zaidi za ushirikiano na maendeleo kwa manufaa ya nchi hizo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, Aprili 17, 2026, alipokutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Patrick Mbundi, aliyefika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha na kuaga rasmi.
Rais Dkt. Mwinyi amemuhakikishia Balozi Mbundi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itaendelea kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu ya pamoja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, na kumtakia kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yake mapya.
Aidha, amesema kuwa wakati nchi wanachama zinajipanga kuimarisha ushirikiano, ipo haja sasa ya kuangalia fursa za utekelezaji wa miradi ya pamoja.
Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Patrick Mbundi, ameahidi kuwa Jumuiya hiyo itaendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na Zanzibar, pamoja na kumpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa mafanikio na maendeleo yanayofikiwa na Zanzibar hivi sasa, ikiwemo kuimarika kwa amani.