Na Albert Kawogo
TAFITI iliyowahi kufanywa mwaka 2006 na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Tanzania Youth Coalition (TYC) kuhusu wimbi la ongezeko la vijana mijini ilikuja na matokeo kwamba, ukosefu wa nishati ya umeme vijijini imechangia kupunguza wigo wa vijana wengi wa vijijini kujiajiri.
Utafiti huo ulibaini kuwa, kama nishati ya umeme ingefika kwenye maeneo mengi ya vijijini basi ingechangia kuzalisha ajira nyingi kwa vijana na akina mama; kwa mfano ziko shughuli za kujiajiri zinazotegemea umeme moja kwa moja kama vile gereji za kuchomea vyuma, saluni, uuzaji, barafu au maji baridi shughuli za steshenari na kazi nyinginezo nyingi.
Kuna ukweli kuwa, vijana wengi hukimbilia mijini kufuata kazi ambazo kama umeme ungekuwepo kwenye maeneo wanayotoka hakika wasingeweza kwenda mjini kuhangaika kutafuta ajira au vibarua ambavyo upatikanaji wake si wa uhakika.

Ndio maana, kwa kutambua umuhimu wa nishati vijijini mwaka 2005 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga sheria ya nishati vijijini (rural energy act No.8 ya mwaka 2005).
Sheria hii ndio iliyopelekea kuanzishwa kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA)ambapo shughuli rasmi za Wakala zilianza mwaka 2007.
REA imeanzishwa ikiwa na lengo kuu ambalo ni kukuza na kurahisisha upatikanaji wa nishati ya kisasa vijijini ili kuboresha maisha ya wananchi na hivyo kukuza uchumi wa maeneo hayo.
Dira ya taifa ya maendeleo ya 2025-2050 na pia ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi CCM 2025-2030 zinaitaja REA kama taasisi muhimu sana kwenye kusimamia usambazaji wa Nishati Vijijini ambao ndio msingi wa kukuza uchumi, viwanda na kuboresha maisha ya wananchi wa vijijini
Hivi karibuni REA kwa kushirikiana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) wamefanya ziara kwenye mikoa ya Pwani, na Njombe ambapo Wahariri hao walipata fursa ya kuona miradi mbalimbali ya gesi na uzalishaji umeme inayoendeshwa na sekta binafsi.

Kwenye miradi hiyo REA imeweza kutoa ruzuku ya kiasi cha Shilingi za Kitanzania Bilioni 16.8 ambazo zimeweza kusaidia ujenzi wa miundombinu na shughuli za uendeshaji.
Mradi wa gesi asilia ulioko eneo la kata ya Kisemvule Mkuranga Pwani ni mfano wa miradi muhimu iliyoweza kufadhiliwa na REA na umeonyesha mafanikio makubwa.
Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa waendelezaji wa mradi kutoka REA Mhandisi Emmanuel Yessaya anasema Wakala ulitenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 6.8 kwa nia ya kufadhili mradi wa usambazaji wa gesi asilia kupitia mfuko wa nishati vijijini (REF) na hatua hiyo imenufaisha kaya 1000 pamoja na taasisi moja.
Kaya hizo kutoka mikoa ya Lindi na Pwani zimesambaziwa miundombinu ya gesi asilia kwa ajili ya kupikia majumbani.
Baadhi ya wanufaika wanasema tangu mradi huo uanze umesaidia sana kupunguza gharama ya maisha kutokana na nafuu wanayopata kwenye kununua gesi ya kupikia.

”Kuuziwa unit moja kwa shilingi 1000 ni sawa na bure tunaishukuru sana REA na pia tunamshukuru Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan,” anasema Mariam Rashid mkazi wa Kisemvule Mkuranga Pwani
Ziara ya Wahariri kutembelea miradi ya REA imefika katika mkoa wa Njombe ambapo fursa ilipatikana kutembelea wilaya za Makete, Njombe na Ludewa kwenye miradi ya uzalishaji umeme na kufadhili usambazaji.
REA katika mkoa huu imeweza kutoa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 10 kwenye miradi mitatu mikubwa.
Baada ya serikali kuruhusu watu binafsi kuzalisha umeme na kuiuzia Shirika la Umeme Tanesco mwitikio huo umekuwa mkubwa kwa mkoa wa Njombe.
Mradi wa Ijangala Min Hydropower Plant ulioko wilayani Makete unazalisha umeme wa maji wa uwezo wa kilowati 360 na kuziingiza katika gridi ya taifa ya Tanesco.

Mratibu wa Mradi huo, Daudi Sanga anasema bila REA wasingeweza kufika hatua hiyo waliyonayo sasa kwani kulikuwa na changamoto nyingi ikiwemo kutokuwa na uwezo hata wa kupata mkopo Benki.
“Kwa kiasi kikubwa mradi wetu umefadhiliwa na REA kwani sehemu ya fedha walizotupa zilisaidia pia kufanya upembuzi yakinifu wa athari za kimazingira ili tuweze kukopesheka Benki,” anasema Sanga.
Mhandisi Yessaya anasema REA kwenye mradi wa umeme Ijangala imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 1.6 ambazo ni ruzuku.
Wahariri pia wamepata fursa ya kufika kwenye mradi mwingine wa uzalishaji umeme wa maji wa Lupali, Lupali Hydropower unaozalisha kilowati 317 na kuingizwa moja kwa moja kwenye gridi ya taifa.
Mradi wa uzalishaji umeme wa Lupali unaendeshwa na Shirika la Watawa wa Kanisa Katoliki la Benedictine Sisters of Gertrud Convent Imiliwaha.

Mhandisi Yessaya anasema REA kwenye mradi huo imetoa ruzuku ya kiasi cha Bilioni 5.4 ambazo ujenzi wa kituo hicho pamoja kujenga miundombinu ya usambazaji kwenye kituo cha Imiliwaha Sisters Convent pamoja na vijiji vya Boimanda, Kitulila na Matola.
Anafafanua kuwa, mradi huo umefikia asilimia 99 na kazi ambazo zimekamilika hadi sasa ni ujenzi wa kizuizi cha maji na mtaro wa kupitisha maji ya mafuriko
Mratibu wa mradi huo Sista Imakulata Mlowe mbali na kuipongeza REA pia anasema mara baada ya mradi huo kukamilika, umeme utakaozalishwa hapo utauzwa moja kwa moja kwa TANESCO ambapo mikataba wa kuuziana umeme umeshasainiwa.
Kwa mkoa wa Njombe REA pia imejipambanua kwenye kusaidia usambazaji wa miundombinu ya kupeleka umeme kwenye vitongoji.

Ziara ya Wahariri inawafikisha katika wilaya ya Ludewa kwenye vitongoji vya ukanda wa Nyasa.
Kwa mujibu wa msimamizi wa miradi ya REA Kanda ya Nyanda za Juu Mhandisi Danstan Kalugira anasema kiasi cha Shilingi Bilioni 3.1 tayari zimeshatolewa na serikali ili kutekeleza mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 6 vya wilaya ya Ludewa.
“Katika mradi huu hapa wilayani Ludewa kampuni ya SUMA JKT ndiye anayetekeleza mradi huu mkubwa ambao unatarajiwa kuunganishia wateja wapatao 160 wa awali mara baada ya mradi kuwa umekamilika,” Anasema Mhandisi Kalugira.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Deodatus Balile ameipongeza REA kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha kuendeleza na kutekeleza miradi mikubwa ya umeme ambayo inakwenda kuleta uhakika wa upatikanaji umeme kwenye mkoa wa Njombe.

Baadhi ya Wahariri waliokuwemo katika ziara hiyo wameonyeshwa kuridhishwa na kazi kubwa ya REA kwenye kusimamia upatikanaji wa nishati ya umeme vijijini.
“Hii village electrification ndio itakayochangia Mapinduzi makubwa ya viwanda vidogo vidogo vijijini na kupunguza tatizo la ajira naipongeza sana REA naipongeza pia serikali kwa hatua hii kubwa,” anasema Idda Mushi kutoka ITV.
Saidi Mwinshehe Mhariri kutoka Michuzi Blog anasema kuona ni kuamini anaipongeza REA huku akisisitiza umuhimu wa ziara za mara kwa mara kama hizi ili Watanzania kupitia vyombo vya habari waweze kufahamu kazi kubwa inayofanywa na REA.