MENEJA wa Mamlaka ya Mapato TRA Mkoa wa Arusha Deogratius Shuma amekabidhi jezi ya Timu ya Mpira wa Miguu ya TRA United, inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania bara kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA Amos Gabriel Makalla leo Jumatatu Machi 09, 2026.
Wakati wa makabidhiano hayo leo Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa Jijini Arusha, Makalla ameipongeza Timu hiyo inayomilikiwa na Mamlaka hiyo kwa kuendelea kufanya vizuri kwenye michezo yake, akihimiza timu hiyo kuendelea kushinda michezo yake na kutokubali kuwa tawi la Timu yoyote ya ligi Kuu.
Amehidi pia kuendelea kuiunga Mkono TRA United, akibainisha pia uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ya viwanja unaotekelezwa Mkoani hapa na serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivyo ni muhimu Timu hiyo kupambana ili kusalia ligi kuu katika kuhakikisha wanaendelea kuutangaza Mkoa na sekta ya utalii hata pale viwanja hivyo vitakapokamilika.
Shuma katika makabidhiano hayo kama ilivyokuwa ahadi yao wakati wa kuipokea Timu hiyo Mkoani Arusha, aliambatana na Uongozi wa Timu hiyo akiwemo Msemaji wake Christina Mwagala.