Na Waandishi Wetu
GENGE la watu wanaotajwa kuwa ni raia wa nchi jirani ya Kongo (majina tunayo) wanadaiwa kuhusika na vitendo vya utapeli kwa wakulima wa mazao mbalimbalii nchini.
Mbali na utapeli huo kwa wakulima hususani wa mazao ya Korosho, mbaazi na mazao mengine, watu hao wanadaiwa kuwatapeli wafanyabiashara wa nchi za Ulaya kwa kuwauzia mizigo hewa ya zao la Parachichi na Iliki.
Uchunguzi uliofanywa na Afrika Leo umebainni kuwa, watu hao wamekuwa wakifanya vitendo hivyo na kujipatia kiasi kikubwa cha fedha huku wakisababisha hasara kwa wakulima na kuichafua nchi Kimataifa.
Moja ya mbinu ambazo wanazitumia kuwatapeli wakulima, ni kuchukua mazao yao kwa kuwatumia madalali waliopo vijijini na kukabidhiwa mazao hayo bila kulipa (mali kauli), kwa ahadi ya kuyasafirisha kwenda nje ya nchi na kulipa fedha baada ya mauzo.
Inaelezwa, wanapochukua mazao hayo, wanayauza ndani ya nchi kwa wafanyabiashara mbalimbali kisha wanatoweka bila kuwalipa wakulima na kuwaachia mzigo madalali waliowadhamini kwa wakulima.
“Wamesababisha matatizo makubwa sana huko vijijini, madalali wanadaiwa kwa sababu wao ndio waliwadhamini wakiamini wakipeleka mazao nje ya nchi watapata faida kubwa, matokeo yake wanauza hapa hapa nchini, wanatoweka na fedha,” alisema Hamis Juma, mkazi wa Tandahimba.
Alisema, wakulima wengi kutokana na elimu ndogo waliyonayo na wengine tamaa, wanarubuniwa kwa kutajiwa faida kubwa, hivyo wanaamua mazao yao hususani Korosho, kuyakabidhi kwa watu hao ambao mwishowe wanatokomea.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa, mbinu nyingine ambayo wanatumia watu hao ambao baadhi yao majina yao na sehemu walipo tunazo, ni kuwahadaa wafanyabiashara wakubwa wanaohitaji kununua Parachichi, ambapo wamekuwa wakipokea fedha bila kuwapatia bidhaa husika.
“Hawa jamaa wana maghala yao kabisa, mteja anapelekwa na kuonyeshwa mzigo, analipia na kuahidiwa atasafirishiwa, lakini kinachotokea jamaa wakishapokea fedha hawatumi mzigo, wengi wamelizwa sana kwa mtindo huu na wanaofanya hivi wanajulikana na wapo,” alisema mkazi mmoja wa Kinondoni ambaye jina lake tunalihifadhi kwasasa.
Mkazi huyo alisema, ameshuhudia watu hao (akimtaja jina mmoja) wakifanya kufuru kwa kuchezea fedha, jambo ambalo limezua gumzo na kusababisha watu kuhoji chanzo cha fedha hizo.
“Wanachezea sana hela, wana maisha ya juu sana na wanaendesha magari ya kifahari mno kwa kazi hii ya kutapeli watu, lakini wanachokifanya ni kibaya sana, kinaichafua nchi yetu na kuwafanya wafanyabiashara wa nje waogope kuja kununua bidhaa hapa nchini,” alisema na kuiomba Serikali kuwachukulia hatua watu hao ili kulinda heshima ya nchi.
Waandishi wa Afrika Leo, walijaribu kuwasiliana na baadhi ya wasemaji wa vyombo vya dola kwa ajili ya kujua kama wanafahamu kuhusiana na suala hilo, lakini jitihada hizo hazikufanikiwa ingawa bado zinaendelea.
Hata hivyo, uchunguzi zaidi kuhusiana na watu hao wanaotajwa kujihusisha na vitendo hivyo vya utapeli wa mazao zinaendelea na taarifa kamili yenye majina yao, picha na mali wanazomiliki itachapishwa kwenye gazeti la Afrika Leo na mtandao huu siku chache zijazo.