ZAIDI ya Shilingi Bilioni 94 zimetumika kuboresha sekta ya elimu katika mkoa wa Manyara ikiwemo ujenzi wa shule maalumu ya Sayansi ya wasichana ya mkoa huo, Shule ya Sekondari ya Wasichana Manyara (Manyara Girls Secondary School) iliyogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 4.7.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Reuben Kwagilwa, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika standi ya zamani Babati Mjini, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, OWM–TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Mwigulu Nchemba wilayani Babati mkoa wa Manyara.
Kwagilwa amesema fedha hizo zimetumika katika kipindi cha miaka minne iliyopita na zimewezesha ujenzi wa shule mpya 26 za sekondari pamoja na shule mpya 65 za msingi, hatua inayolenga kupanua wigo wa elimu na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Shule za Sayansi kwa wasichana, zimeleta mapinduzi makubwa kwa watoto wa kike na hasa kwenye masomo ya sayansi ambayo kama Taifa kumekuwa na upungufu wa wanafunzi wanaosoma masomo ya Sayansi,” amefafanua Kwagilwa.
Akisisitiza kuhusu maboresho ya sekta ya elimu, Kwagilwa amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu nchini ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira bora na kwa utulivu jambo litakalosaidia kuongeza ufaulu na kuandaa rasilimali watu yenye ushindani.