📌 Minara 1,041 Yajengwa Ndani ya Miaka Minne
SERIKALI kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema kuwa inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuboresha na kusogeza huduma za mawasiliano kwa wananchi, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini na pembezoni mwa nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Zacharia Mkama wakati akijibu swali la Eng. Fadhili Sandali Chilombe, Mbunge wa Tunduru Kusini aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali wa kujenga minara ya mawasiliano katika vijiji vya Kazamoyo, Imani na Kilimani.
Dkt. Mkama alieleza kuwa katika kipindi cha Miaka Minne (4), Serikali imejenga jumla ya minara 1,041 ya mawasiliano.
Kati ya hiyo, minara 758 imejengwa kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidigitali, ambao ulizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 13 Mei, 2023, ukiwa na lengo la kuhakikisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano unaimarika nchini kote.
Dkt. Mkama alisema kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa.
Alieleza kuwa Disemba 5, 2025, mikataba ya utekelezaji wa miradi ya mawasiliano katika kata 201 ilisainiwa, ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2027.
Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2025/2026, Serikali kupitia UCSAF imepanga kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo mengine 280, yakiwemo maeneo ya kimkakati kama reli ya kisasa (SGR), hifadhi za Taifa, barabara kuu na maeneo ya mipakani.
Akizungumzia mkakati wa muda mrefu, Mhe. Dkt. Mkama alisema kuwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na taasisi zake pamoja na Makampuni ya Simu, inaandaa Mkakati wa Kitaifa wa Miaka Mitano (2025–2030) wa ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu, wenye lengo la kumaliza au kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini.