▪️Asisitiza Taasisi za Serikali zinapaswa kufahamu kwamba
makao makuu ya nchi ni Dodoma
WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Serikali inataka kazi zote zifanyike makao makuu ya nchi ili kusogeza huduma karibu na Wananchi.
Amesema hayo leo Alhamisi (Januari 22, 2026) alipotembelea Ofisi za Wizara ya Maji na Wizara ya Madini zilizopo mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.
“Ninawapongeza sana, mmehamia Makao Makuu, taasisi zote za Serikali zinapaswa kutambua kwamba makao makuu ya nchi ni Dodoma, na huduma zote zinapaswa kutolewa hapa, hii sio kambi na wala hatutakuwa na Makao Makuu mbili zilizo sambamba”.
Pia, Mwigulu ameziagiza Taasisi zote ambazo zimeshakamilisha ujenzi wa majengo katika makao makuu kuyatoa majengo hayo kwa Taasisi ambazo haziwajibiki kuhamia Dodoma lakini bado zimepanga.
“Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu mwelekeze Katibu Mkuu atengeneze timu ifanye tathmini ya majengo yote ya Serikali yaliyoko Dar es Salaam ambayo hayana matumizi ili tuyagawe kwa taasisi nyingine ambazo zimepanga, angalia Serikali ina majengo yasiyotumika”
Kadhalika Waziri Mkuu amesema kwa kuwa Ofisi za Serikali zipo karibu, hivyo hakuna haja ya kuandikiana barua za masuala mbalimbali ya utekelezaji badala yake waweke mpango wa kutembeleana katika ofisi husika ili kutatua jambo lilikokwama kwa wakati”
Akizungumza na Watumishi wa Wizara ya Maji Dkt. Mwigulu amewataka kwenda katika hatua ya kukomesha kabisa upotevu wa maji.
“Tunapokwenda kutekeleza dira mpya tunatakiwa twende na ustaarabu na miundombinu inayomuhakikishia mtanzania uhakika wa kupata maji”
Akizungumza wakati akikagua majengo ya Wizara ya Madini, Dkt. Mwigulu amewataka wataalam wa madini kuendeleza jitihada kwenye tafiti za madini ili kujua utajiri uliopo nchini.