Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KATIBU wa Kamati Maalum NEC, Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis amewataka vijana wa kizazi cha sasa maarufu kama GEN Z kuwa wazalendo na nchi yao, kujiandaa kushika madaraka na kujifunza historia ya nchi yao.
Mbeto alisema, vijana hawapaswi kufuata mkumbo, badala yake wafuate nyayo za viongozi waliopita ambao kabla ya mapinduzi walikuwa vijana na walisimama imara kuipigania nchi yao na kuipitisha kwenye misukosuko iliyojitokeza baada ya mapinduzi.
“Sayansi inasema mzee atatangulia mwanzo, kijana atabaki. Ndio maana wazee wengi tunahangaika kuwatafutia watoto wetu tukiamini sisi tutatangulia, wao watabaki, kwa maana hiyo tunapaswa kuwa kizazi kinachojielewa na wazalendo, wasiwe vijana wanaofitini nchi yao,” alisema.
Aliendelea kusema: “Ukiwaangalia akina Mzee Karume, Nyerere walianzisha mapambano yao wakiwa vijana, miaka 28 mtu anaaminiwa kuwa Waziri Mkuu wa nchi, alikuwa kijana mdogo, lakini alikuwa anajielewa, hakutumika vibaya wala hakuwa chawa, na siku hizi vijana tunaumizana, tunatiliana fitna kwa hofu tu fulani atakuwa fulani,”
Mbeto alisema, viongozi hao walipendana, walikaa pamoja na kupanga mipango ya kuikomboa nchi yao, lakini ni tofauti na hivi sasa vijana wengi wanasubiri mwenzao mambo yake yaharibike.
“Vijana tujifunze kwa walioratibu Mapinduzi na kufanikiwa, walifanya jambo kubwa ambalo mpaka leo sote tumegomboka, kwahiyo nasisi tuache alama ya kupendana na kusaidia nchi yetu na sio kutumika kuiharibu,” alisisitiza Mbeto.
Aidha, aliitaka Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) kuunganisha vijana na kuachana na vitendo vya kuhujumiana ili warithi uongozi wakiwa wameiva, ikizingatiwa kwamba viongozi waliopo sasa madarakani Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Mwinyi wanawapa nafasi kubwa vijana kwa ajili ya kuwajenga.
“Usitarajie atakuja kiongozi mwingine ambaye atashika madaraka mwenye umri zaidi ya Dkt. Mwinyi, tutakaoshika hatamu ya nchi hii ni sisi vijana, kizazi cha akina Mzee Shein hawapo tena, maana yake ni kwamba nchi inakuja moja kwa moja kwetu, kwahiyo tujiandae vizuri kupokea hayo Madaraka,” alisema.
Mwenezi Mbeto alisema, anaamini zitakapoanza chaguzi za nafasi mbalimbali ndani ya Chama cha Mapinduzi, wakaojitokeza zaidi ni vijana, hivyo ni vema wakajiandaa na kuwaonyesha wazee ambao bado wapo kwamba, iwapo watapewa dhamana ya kuongoza nchi, wataipeleka salama na wakamaliza umri wao wakiwa salama.
Mbali na hilo, aliwataka vijana hao kujifunza historia ya nchi yao ili wasipotoshwe na baadhi ya watu ambao wanaleta chokochoko kwa lengo la kubeza Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambayo lengo lake lilikuwa ni kuleta usawa kwa watu wote ili kila mmoja anufaike na matunda ya nchi yake.
Mbeto alisema, katika kutekeleza malengo ya mapinduzi, viongozi waliopita na aliyepo sasa Dkt. Hussein Mwinyi amefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuhakikisha huduma mbalimbali zinapatikana kwa usawa, karibu na wananchi na kwa ubora, ambapo kwenye suala la elimu, afya na kwingineko yamefanyika mambo mengi ambayo yataacha alama kwa kiongozi huyo baada ya kumaliza muda wake.