Vijiji 1,407 vyafikiwa na mawasiliano
SERIKALI kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imekamilisha ujenzi wa minara yote 758 kati ya 758, mradi mkubwa wa kimkakati uliotekelezwa kwa kipindi cha takribani miaka miwili kwa lengo la kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini, hususan katika maeneo ya vijijini na pembezoni.
Kukamilika kwa mradi huo kumewezesha zaidi ya wananchi milioni 8.5 wanaoishi katika vijiji 1,407 kupata huduma za mawasiliano ya simu na intaneti, hatua inayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kuboresha upatikanaji wa huduma za elimu, afya, biashara na usalama, pamoja na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika uchumi wa kidijitali.
Ujenzi wa minara hiyo umefanyika kwa ushirikiano kati ya Serikali na watoa huduma za mawasiliano nchini, ambapo Serikali kupitia UCSAF ilitoa ruzuku ya shilingi bilioni 126 kwa makampuni ya simu ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo.
Kupitia mradi huu, UCSAF inaendelea kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za mawasiliano kwa usawa, kama nyenzo muhimu ya maendeleo, ubunifu na ustawi wa taifa kwa ujumla.