Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis
Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Othman Masoud Othman kuacha porojo na kuwapotosha wananchi kwa kupandikiza maneno ya hasama na chuki katika jamii huku akiahidi mambo yasiyowezekana.
Vile vile, CCM kimesisitiza kuwa Uchaguzi Mkuu umeshamalizika, wananchi wametumia haki yao ya kikatiba na kidemokrasia kwa kuiweka Serikali walioitaka madarakani.
Matamshi hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis aliyemtaka Othman kukubali ukweli ameshindwa Uchaguzi kutokana na nguvu ya maamuzi ya wengi.
Mbeto alisema, Othman hana sababu zenye mashiko, bali anajaribu kuidanganya dunia akidai yeye ndiye mshindi wakati Tume ya Uchaguzi Zanzibar imeshamtangaza mgombea aliyeshinda Urais.
Alisema Othman asingeweza kumshinda mgombea wa CCM Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa sababu kadhaa muhimu ambazo zina ukweli usiokwepeka.
“Othman alikuwa akiomba nafasi ya kuchaguliwa ili awatumikie wananchi wa Zanzibar. Rais Dkt. Mwinyi alishapimwa jinsi alivyoitumikia nchi na watu miaka mitano iliyopita. Ndoto ya OMO ni kuleta Maendeleo wakati mwenzake alishafanya kazi ya kuleta maendeleo yanayoonekana,” alisema Mbeto.
Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisema fikra na hesabu za Othman alidhani wananchi wangembagua na kumchukia Rais Dkt. Mwinyi kutokana na matamshi ya Makamu wake Mwenyekiti Ismail Jussa Ladhu alivyokuwa akitumia hotuba za ubaguzi kama sera na mtaji wa kupata ushindi.
“Zanzibar nchi ya Visiwa. Ni mkusanyiko na mkutanisho wa watu toka pembe nyingi za dunia. Unapoonyesha au chama chako kina sera za kibaguzi unalazimisha upigiwe kura za chuki dhidi yako,” alieleza.
Pia, Mwenezi huyo alisema miaka mitano iliyopita utawala wa Rais Dkt. Mwinyi umewaunganisha wananchi waliogawanyika kwa siasa za chuki, ambapo ameongoza bila kujali asili zao, rangi walizonazo, Siasa au itikadi za vyama vyao.
“Kwa miaka mitano iliyopita Wazanzibari waliishi kwa utulivu kama maji ndani ya mtungi. Wamekuwa wamoja, wenye upendo mshikamano. Hazikusikika sauti za kubaguana, kusimangana wala kuhitilafiana,” alisisitiza.
Mbeto alimtaja Jussa kuwa ndiye kiongozi pekee ambaye kila wakati alisikika katika mikutano yake akijaribu kuwagawa wananchi kwa asili zao, nasaba na siasa ili kuwavuruga kwa historia na matukio ya kisiasa yaliyopita.
“Kushindwa kwake OMO kwa sehemu kubwa kumeporomoshwa na aina ya utata wa Siasa na matamshi ya Jussa. Wazanzibari wamechoshwa na heka heka za kubaguana na kugombanishwa kwa itikadi za vyama,” alisema Mwenezi huyo.