NAIBU Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Reuben Kwagilwa, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Pwani kuendelea kubuni miradi mipya itakayoongeza vyanzo vya mapato ya mkoa.
Akizungumza katika kikao kazi na watendaji wa mkoa huo, Kwagilwa amepongeza hatua za ukusanyaji wa mapato pamoja na usimamizi mzuri wa matumizi, akisisitiza kuwa mkoa unapaswa kuendeleza kasi hiyo ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma kwa wananchi.
Katika ziara yake iliyofanyika Novemba 29, 2025, Naibu Waziri amekagua hatua za ujenzi wa Shule ya Watoto Wenye Mahitaji Maalum Mlandizi, na kutoa maelekezo kwa mkandarasi kuhakikisha mradi huo unakamilika kabla ya Januari 2026.
Aidha, Mhe. Kwagilwa ameagiza majengo yote ya taasisi za Serikali zilizo chini ya TAMISEMI yapimwe na kupatiwa hati miliki, ili kuongeza ulinzi wa mali za umma na kuwezesha matumizi sahihi ya ardhi.
Mradi wa shule hiyo, wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 500, unatekelezwa katika mwendelezo wa kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Sita ya “Kazi na Utu”, inayolenga kuimarisha huduma jumuishi na uwezeshaji kwa makundi maalum.


