Rais Mwinyi asisitiza umuhimu wa amani kwa maendeleo ya Taifa

0

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, kuna umuhimu mkubwa kwa kila Mwananchi kutimiza wajibu wake katika kudumisha Amani.

Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa makundi ya Wanasiasa, Viongozi wa Dini na Waandishi wa Habari kuwa makini na kauli wanazozitoa mbele ya jamii kwa kuwa ndio makundi yanayosikilizwa na watu wengi na yenye ushawishi mkubwa katika jamii.

Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipojumuika na Waumini wa Dini ya Kiislamu katika Sala ya Ijumaa na Dua Maalumu ya Kumshukuru Mungu pamoja na kuiombea Taifa Amani.

Dua hiyo imesomwa katika Msikiti wa Jamiu Zinjibar, Kiembe Samaki, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amefafanua kuwa matukio yaliyojitokeza Tanzania Bara ni funzo muhimu kwa Watanzania wote, ikiwemo Zanzibar, kwamba hakuna jambo linaloweza kufanikiwa bila kuwepo kwa Amani katika nchi.

Ameeleza kuwa si suala la maendeleo pekee bali hata ibada haziwezi kufanyika panapokosekana Amani.

Amewasisitiza Wanasiasa, Viongozi wa Dini na Waandishi wa Habari kuendelea kuhubiri na kuimarisha Amani wakati wote.

Rais Dkt. Mwinyi amewataka Viongozi wa Dini zote kuwa na kauli zinazohimiza Amani kwa wafuasi wao, na kuwataka Waandishi wa Habari kutumia kalamu zao na mitandao ya kijamii kwa busara, na kuacha kuchapisha habari zinazoathiri Amani ya nchi.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru Afisi ya Mufti kwa kuandaa Dua hiyo maalum ya kuiombea nchi Amani na kumshukuru Mungu kwa kuijalia Nchi utulivu kabla, wakati na baada ya Uchaguzi.

Akitoa salamu za Afisi ya Mufti, Katibu Mtendaji Sheikh Khalid Ali Mfaume amewahimiza Wananchi wa Tanzania, ikiwemo Zanzibar, kuithamini na kuipenda Nchi yao kwa kuwa ndio Taifa walilobarikiwa na Mwenyezi Mungu.

Amesisitiza kuwa kila mmoja, hususan Vijana, wanapaswa kulithamini Taifa lao na kuishi maisha yenye Nidhamu na Hekima kila siku.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here