Na Mwandishi Wetu
KATIBU wa Kamati Maalum NEC, Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis amewataka vijana nchini kutokubali kuchochewa na watu wasioitakia mema nchi na kuvuruga amani ambayo ni moja ya tunu ya Taifa.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake, CCM Kisiwandui, Mbeto alisema, Tanzania bado ni kimbilio kwa watu kutoka nchi mbalimbali, hivyo yakitokea machafuko athari inakuwa kubwa na inawagusa wengi.
Alisema, siku chache ambazo kulitokea vurugu za maandamano yaliyofanyika kwenye baadhi ya maeneo ya Tanzania Bara, shughuli nyingi za kiuchumi zilisimama na hakukuwa na biashara iliyofanyika.
“Niwaombe sana vijana, msichochewe na jazba za watu wasioitakia mema nchi yetu, wakatuingiza kwenye chaka,” alisema na kuongeza kuwa, amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuwa vinara wa kuchochea fujo nchini kwa kutumia mitandao ya kijamii.
Alisema, watu hao wanapaswa kujua kwamba, wao na watoto wao wanaishi nje ya nchi, lakini ndugu zao wengine wapo nchini, hivyo kukitokea machafuko nao wataathirika.
“Usikubali kutumiwa kwa fedha chache ukaharibu amani, umoja na mshikamano wa nchi yetu,” alisema Mbeto na kuwapongeza Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha amani inaendelea kuwepo na shughuli za kawaida zinaendelea.
Mbeto aliwasihi watanzania kuendelea kuitunza amani, huku akisisitiza kwamba ‘sumu haionjwi’ na kuwataka kutoiga yanayoendelea kwenye Mataifa mengine ambayo yameingia kwenye machafuko.
“Ushindi wa Rais Samia ni ushindi wa Watanzania wote, ushindi wa Dkt. Mwinyi ni ushindi wa Wazanzibar wote, tushikamane, tuwape mashirikiano viongozi wetu, waendelee kuitumikia nchi yetu, waendelee kutuletea maendeleo,” alisema Mbeto na kuongeza kuwa, iwapo kuna mambo hayapo sawa, ni vema kukaa chini na kuyazungumza.