Na George Uledi
WANAHARAKATI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walio nje ya nchi (Sweden Kenya na Marekani) wakishirikiana na viongozi wa chama hicho ndani ya nchi, wamekuwa kwenye utekelezaji wa ‘mradi’ wao ovu wa kuhakikisha wanafanya kila wanaloweza kuiingiza nchi kwenye machafuko.
Baada ya chama hicho kushindwa kuwashawishi wananchi wawachague kupitia sanduku la kura, njia pekee wanayoamini inaweza kuwasaidia kuingia madarakani ni kuchochea uasi, kutokee umwagaji damu na wao waingie madarakani, jambo ambalo vyombo Ulinzi na Usalama na watanzania hawapo tayari kuona likitokea.
Mradi huu umekuwa ukijaribiwa kwenye kila utawala; itakumbukwa jinsi walivyopambana kupitia kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya vyombo vya Habari na majukwaa ya kisiasa kuchafua utawala wa Awamu ya Nne uliokuwa chini ya Dkt. Jakaya Kikwete.
Ni wanaharakati hao kwa kushirikiana na Chadema, walitoa taarifa mbalimbali za kutaka kuuaminisha umma na Jumuiya za Kimataifa kwamba, licha ya watanzania kuwa kwenye hali ngumu kiuchumi, lakini viongozi wanakula raha, wakiamini suala hilo linaweza kuibua hasira za wananchi hao na kuingia barabarani kufanya maandamano na vurugu.
Tulishuhudia maandamano na vurugu za hapa na pale ambazo zilisababisha vifo na uharibifu wa mali; Chadema wakatumia nafasi hiyo kupiga picha na kuzitembeza kwenye nchi mbalimbali ili kushawishi waungwe mkono na ikibidi nchi iwekewe vikwazo na hatimaye yafanyike mabadiliko ya uongozi.
Utawala uliofuata wa Awamu ya Tano, uliokuwa chini ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, nao ukakumbwa na misukosuko mingi, wanaharakati hao wakatangaza kwamba nchi sio salama; kwamba mbali na hali ngumu ya maisha wakitumia neno vyuma ‘vimekaza,’ kumekithiri utekaji na mauaji, kwamba hali ya Uchumi ni ngumu, hivyo watanzania wanatakiwa kufanya mabadiliko.
Mara baada ya kifo cha Dkt. Magufuli, akaingia Rais Dkt. Samia ambaye alijitahidi kwa kiasi kikubwa kurekebisha yale ambayo yalikuwa yanalalamikiwa na wapinzani na akafikia hatua ya kuunda tume mbalimbali za kuchukua maoni na kushauri namna bora zaidi ya kufanya siasa za nchi akitumia falsafa yake ya 4R.
Yapo ambayo yalifanyiwa kazi kwa haraka, ndio maana ikafikia hatua wanasiasa ambao walikimbia nchi, walirejea na baadhi ya madai yao yakatekelezwa na wakapongeza mwenendo wa nchi ikiwemo wanasiasa wa vyama vya upinzani kuruhusiwa kufanya mikutano ya kisiasa.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, wale wale ambao walimpongeza Rais Samia, wamegeuka na kuuponda utawala wake na kila kunapokucha, wamekuwa wakizusha mambo kwa lengo la kujenga chuki ili wauchukie utawala wake. Wakati fulani, walitumia mikutano waliyoruhusiwa kufanya siasa za majitaka; kumtukana Rais na kufanya uchochezi badala ya kutangaza sera zao.
Chadema ili kuhakikisha wanateteresha utawala wa Rais Dkt. Samia, wakaja na mkakati wa ‘No Reforms No Election,’ ambao unaendelea kuchochewa kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29, 2025, ingawa kuna dalili zote umeshindwa kabla ya kufanyika.
Malengo makuu ya mkakati hu; ni kuhamasisha maandamano, kuvuruga uchaguzi mkuu, kuishinikiza Serikali kufanya mabadiliko ya lazima ambayo wanayataka wao ikiwemo Katiba Mpya na mengineyo.
Ili kufanikisha mkakati huo, Chadema walijipanga kuchonganisha vyombo vyetu vya ulinzi na Usalama (JWTZ, Jeshi la Polisi). Wakasema Jeshi la Wananchi (TPDF) lipo nyuma ya wananchi, hivyo watu wengi watoke Oktoba kwenda kwenye Maandamano, na kwamba hakuna Polisi atakayewagusa.
Baada ya kuona JWTZ limekataa kuwa sehemu ya siasa kupitia kwa Kaimu Msemaji wake ambaye alitoa taarifa kwa umma, wakachanganyikiwa kwa kuvurugika kwa mipango yao.
Ikumbukwe, lengo lilikuwa ni kupata uungwaji mkono wa wananchi ili wajitokeze kwenye maandamano wakiamini wana nguvu ya JWTZ, lakini mambo yakawa tofauti.
Mkakati wa pili wamekuja nao hivi karibuni; ni kuwatisha wananchi ili wasiende kupiga kura Oktoba 29, 2025 kwa kuzusha kwamba, kuna wanajeshi zaidi ya 500 wameingia nchini kwa ajili ya kuzuia maandamano, hivyo wanaweza kuteka na kuwaua watu watakaokwenda kupiga kura.
Lengo la mpango huu ni kuwatisha wapiga kura ili wasitoke siku ya Uchaguzi na kuwajengea hofu ionekane kuna tishio kubwa la usalama, suala ambalo Rais Dkt. Samia amesema halipo na kuwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura.
Kwamba, siku hiyo hakutakuwa na maandamano yoyote zaidi ya yale ya kwenda kwenye vituo vya kupigia. Vile vile, JWTZ kupitia kwa viongozi wake waliweka wazi kwamba, nchi ipo salama, hivyo mpango wao wa kuvigawa vyombo vya Ulinzi na Usalama umekwama.
Yote haya yanakuja baada ya ukweli kwamba, tayari maandamano wanayotarajia yafanyike Oktoba 29, yameshindwa mapema na walichobaki nacho ni kutengeneza uzushi. Ikumbukwe, wakati fulani waliwahi kusambaza uongo kwamba kuna shehena kubwa ya silaha imeingizwa nchini kwa ajili ya kuwadhuru watanzania.
Hata hivyo, jambo hilo limebainika halina ukweli wowote, haliwezekani na lilitungwa kwa ajili ya kutengeneza taharuki kwenye jamii, suala hilo nalo likapuuzwa na kupita, sasa wamekuja na mpya ambayo nayo siku chache zijazo itapotea kwenye masikio ya watu.
Ukiwasikiliza wananchi walio wengi hivisasa, wanaonekana wazi kuchoshwa na uzushi unaosambazwa na watu hao wasioitakia mema nchi ikizingatiwa wote wanatunga mambo hayo, wapo nje ya nchi na familia zao, hivyo kukitokea machafuko watabaki salama.
Kwa mfuatiliaji mzuri wa mikutano ya kampeni inayoendeleea hivi sasa, atagundua kwamba, mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan, mikutano yake inaongoza kwa kupata watu wengi.
Hiyo ni dalili tosha kwamba, wapo tayari kushiriki zoezi la kupiga kura, na msemo wa ‘Oktoba Tunatiki,’ umekuwa maarufu na upo karibu na vinywa vya watanzania wengi, jambo ambalo limewatisha waratibu wa maandamano.
Dalili za kushindwa kwa mkakati wa kufanya vurugu wakati wa uchaguzi unaonekana wazi kupitia kauli za wahamasishaji wa maandamano hayo ambao awali walisikika wakiwataka watanzania washiriki maandamano, lakini hivi sasa wanachohubiri zaidi ni kuwazuia watu wasiende kupiga kura.
Ni wazi wanaona kuwa, ‘No Reforms No Election’ kwa sasa haiwezekani kabisa, kwani walitaka siku ya kwenda kupiga kura, ndio iwe siku ya maandamano, lakini jambo hilo nalo linaelekea kufeli, hivyo jambo pekee lililobaki ni kuwazuia wasiende kupiga kura kwa vitisho vya kuingia nchini kwa wanajeshi 500 wa Uganda, shehena za silaha na mengineyo ambayo hayaingii akilini.
Tujiulize, kama wanajeshi wa Uganda 500 wameingia nchini, wapo wapi hadi wasionekane? Achana na idadi hiyo kubwa ya wanajeshi kuingia nchini, hata kuku 500 hawawezi kuingia Tanzania wasionekane. Ukiachilia mbali hilo, Tanzania ina wanajeshi wengi nje ya nchi wakitekeleza majukumu ya kulinda amani, Rais Samia angeshindwa kuwarudisha hadi akakodia Jeshi la Uganda?
Yaani, tuna Jeshi la Polisi, JWTZ, Jeshi la Magereza, Jeshi la Uhamiaji, Zimamoto na TISS, vyombo vyote hivyo vishindwe kuzuia maandamano mpaka twende Uganda? Uongo mbaya sana!
Ni hivi. JWTZ lipo imara na tayari kwa tishio la aina yoyote lile na wala halijawahi kuwaza na alitowaza kuomba msaada kokote hasa katika jukumu la kudumisha ulinzi wa mipaka na uhuru wa nchi hii.
Kama alivyoahidi Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kauli za vyombo vyetu vya dola kuhakikisha usalama wa raia, mali zao na mipaka ya nchi, nawasihi wote wenye sifa za kupiga kura, twende kifua mbele tukatumie haki yetu ya kikatiba, kisha turudi majumbani kusubiri matokeo, tuwapuuze wanaharakati na wanasiasa uchwara wanaotaka kuingia madarakani kwa kutumia damu za watu, hawana jipya.