Na Mwandishi Wetu
VIONGOZI, wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa muda mrefu wamekuwa wakijitangaza ili jamii iwaone kwamba, ni chama ambacho hakina doa na wala hakijawahi kujihusisha na matukio yoyote ya uhalifu, hivyo wao ndio wenye Mamlaka ya kutuhumu wengine hata kama hawana ushahidi.
Hata hivyo, historia inaonyesha yapo matukio ya kutisha ambayo yalifanyika, wapo baadhi ya viongozi wao wengine hadi sasa wapo kwenye chama hicho, walikamatwa, wakafikishwa mahakamani, lakini hadi leo hazijulikani hatma yake.
Yapo madai kwamba, sababu ya kesi hizo kufumbiwa macho, ni kutokana na busara za viongozi; vinginevyo viongozi wengi wa chama hicho wangekuwa wamechukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kuhukumiwa kifungo jela.
Kwasasa, ukiwasikiliza viongozi hao na wanachama, wanazungumzia suala la kutekwa na kuumizwa watu, ni kama suala jipya, lakini ukweli ni kwamba, limekuwepo tangu miaka ya nyuma na chama hicho kilishapoteza uhalali wa kukemea suala hilo kwasababu wao ni waasisi wa matukio hayo.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, kwenye uchaguzi mdogo wa Igunga uliofanyika mwaka 2011, baadhi ya wanachama wa chama hicho kutoka Makao Makuu jijini Dar es Salaam, walituhumiwa kummwagia tindikali mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mussa Tesha wakati wa maandalizi ya kampeni za uchaguzi huo wa kuziba nafasi ya aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo Rostam Aziz, ambaye alitangaza kuachana na siasa.
Nimewahi kuzungumza na Mussa Tesha kuhusu tukio hilo, anasema wazi waliomtendea unyama huo na kumuumiza vibaya hadi kumsababishia ulemavu wa kudumu, ni wafuasi wa Chadema na anawataja kwa majina na kutaja namba na aina ya gari ambalo linadaiwa kutumika kumteka na kumpeleka nje ya mji wa Igunga; gari ambalo anasema ni mali ya mmoja wa viongozi wa chama hicho.
Kijana huyo anasema, wafuasi hao baada ya kumkuta akitekeleza majukumu yake aliyopewa na chama chake, walimzunguka na kumchukua kwa nguvu, wakamuingiza kwenye gari na kuondoka naye; njiani walimpa vitisho vingi na hatimaye walipofika kwenye eneo walilopanga kufanyia unyama huo walimshusha, wakampiga, kisha walimmwagia tindikali usoni na kumtelekeza kabla ya kusaidiwa na wasamaria wema waliomkuta akiwa kwenye hali mbaya.
Baada ya tukio hilo, kukazuka taharuki nyingine; ni baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Temeke Joseph Yona, kuokotwa maeneo ya Ununio akiwa na majeraha mengi usoni huku akiwa hajitambui.
Yona baada ya kupata nafuu kutokana na matibabu aliyoyapata, alipohojiwa alisema waliomteka na kumpiga na kisha kumtupa Ununio ni wanachama wenzake wa Chadema.
Yona alifanyiwa unyama huo wakati ambapo Chadema walikuwa kwenye mgogoro mkubwa uliodaiwa kuzuka baada ya kubainika kumeundwa kundi linaloitwa Masalia (PM7), likihusishwa na Zitto Kabwe ambaye alikuwa kiongozi wa chama hicho kabla ya kuvuliwa uanachama na kuhamia ACT- Wazalendo, ambapo Yona alikuwa mmoja wa wafuasi wake.
Inadaiwa, kila ambaye alikuwa mfuasi wa kundi la Masalia ambalo lilipanga kufanya mabadiliko makubwa ndani ya chama hicho, alidhibitiwa na inasemekana waliomteka Yona, walikuwa kwenye harakati hizo za kuhakikisha wanazima nguvu ya kundi la Masalia ambalo baadae lilisambaratika baada ya wafuasi wake wengine kufukuzwa na wengine walijitoa Chadema kabla ya kufukuzwa.
Mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru, Christopher Lissa naye hawezi kuwasahau walinzi wa Makao Makuu ya Chadema. Yeye alivamiwa wakati alipokwenda kwenye ofisi hizo baada ya kusikia kuna wanachama wa chama hicho wamepanga kuandamana, hivyo alikwenda kufuatilia habari hizo akiwa na waandishi wenzake wa vyombo mbalimbali vya habari.
Lakini, cha kushangaza mwandishi huyo alivamiwa na walinzi wa Chadema, wakamshambulia kwa ngumi, wakampiga kwa magongo na vyuma huku wakimshinikiza akiri kuhusika kuandaaa maandamano hayo, hata hivyo taarifa zilisambaa haraka na mwandishi huyo akapata msaada akiwa kwenye hali mbaya.
Khalid Kagezi, mlinzi wa zamani wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema Balozi Dkt. Wilbroad Slaa, naye ana simulizi ya mateso aliyoyapata baada ya kutekwa na kuwekwa ndani ya chumba maalumu cha mateso na watu ambao anawajua na hata kwenye mkutano wake na waandishi wa habari alioufanya baada ya kunusurika, aliwataja kwa majina na wengine ni viongozi wa chama hicho.
“Chadema waliniteka na kunifungia kwenye chumba cha mateso wanachomiliki wao, wamenichoma visu na kuniweka kwenye mashine ya umeme bila kosa lolote, eti wakinishinikiza nitaje wanaonituma,” alisema Kagezi huku akionyesha majeraha ya visu alivyochomwa mgongoni.
Ukiachilia mbali hao waliotekwa na kupata mateso makubwa, kwenye kila chaguzi tangu mwaka 2010 Chadema wamesababisha matatizo makubwa kwa watu wengi; wapo waliopoteza maisha kutokana na vurugu walizochochea, wapo waliofungwa kwa kuvunja sheria za nchi kwa sababu ya kufuata kauli za viongozi wa Chadema.
Wengine wamepata ulemavu wa kudumu kwa kuingizwa kwenye vurugu ambazo zilichochewa na viongozi wa chama hicho; mfano mzuri ni zile za kupinga ushindi wa Meya wa Arusha, zilizotokea baada ya uchaguzi Mkuu wa 2010 ambapo mgombea wa Chadema alishindwa.
Kufuatia matokeo hayo, viongozi wa Chadema waliwachochea wafuasi wao kufanya maandamano yasiyo na kibali ambayo yalitawanywa na kisha baadhi yao walikamatwa, lakini baadae viongozi hao walitoa agizo kwa wanachama na wafuasi wao waende kwenye kituo kikuu cha polisi, kuwatoa kwa nguvu watuhumiwa hao.
Katika kutii agizo hilo, kundi kubwa la wafuasi wa Chadema lilielekea yalipo Makao Makuu ya polisi kwenda kutekeleza kazi waliyotumwa, matokeo yake kukatokea mapambano makali kati ya raia na polisi na kusababisha vifo vya watu watatu.
Mbali na tukio hilo, mjini Morogoro nako kijana Ali Zona alipoteza maisha wakati wa maandamano haramu yaliyohamasishwa na viongozi wa Chadema.
Kijana huyo awali ilielezwa alipigwa risasi na polisi, lakini baada ya uchunguzi ambao uliwahusisha baadhi ya viongozi wa Chadema mkoani hapo, ikabainika alipigwa na nondo kichwani, haikuwa risasi kama ilivyodaiwa.
Haya ni machache, yapo matukio mengi ambayo unaweza kuandika hata kitabu kuyaelezea na bado yasitoshe, lakini itoshe kusema kwamba, busara iliyotumika kuwafumbia macho wanachama na viongozi wa chama hiki, huenda ndio imechangia Chadema kupata ujasiri wa kusimama mbele ya umma na kujipa uhalali wa kumtuhumu kila mtu, ikiwemo Serikali na wakati mwingine kwa matukio ambayo hayana ukweli.